27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

KWAHERI MZEE KINGUNGE, ULIKUWA KIUNGO MUHIMU

USIKU wa kuamkia jana Taifa lilipatwa na msiba wa kuondokewa na mmoja wa wazee na wanasiasa mashuhuri, Kingunge Ngombale Mwiru.

Tunasema Tanzania inalia kwa kumpoteza mmoja wa wazee wake, kwa kuwa alitegemewa kwa ushauri na busara zake katika kuliongoza Taifa hili bila kujali tofauti zetu za rangi, makabila, kanda, itikadi au tofauti za kiuchumi.

Kingunge alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa tangu ashambuliwe na mbwa Desemba 22, mwaka jana. Kingunge ni maarufu katika siasa za Tanzania na anakaribiana na wazee wengine waliotangulia mbele za haki akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Rashid Kawawa, Oscar Kambona, George Kahama na wengine wengi ambao Taifa litaendelea kuwalilia kila siku kutokana na mchango mkubwa na uadilifu wao.

Nasi MTANZANIA Jumamosi tunaungana na Watanzania wote kuuenzi utumishi uliotukuka wa Kingunge kwa Taifa hili tangu enzi za chama cha Tanu, Uhuru na baada ya Uhuru. Katika salamu zake za rambirambi kutokana na msiba huo, Rais Dk. John Magufuli, alisema Taifa haliwezi kumsahau Kingunge.

Tunawaomba Watanzania wote kuyaenzi mema yote aliyofanya Kingunge wakati wa utumishi wake. Ametuachia somo kubwa la kujali masilahi ya nchi wakati wote.

Kingunge ametufundisha pia kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu. Licha ya kuitumikia Serikali kwa muda mrefu, Kingunge pia alikuwa mbunge kwa miaka mingi. Pia alikuwa mjumbe wa Bunge la Katiba mwaka 2014.

Tunaamini kwamba, wengi watakuwa ni mashahidi jinsi Kingunge alivyotoa mchango wake katika mchakato ule kwa busara na umahiri mkubwa. Tunasema Kingunge alikuwa kiungo muhimu kati ya makundi mbalimbali ya kijamii.

Pia alikuwa daraja kati ya wanasiasa wa upinzani na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tunamkumbuka Kingunge kama mtu aliyetegemewa kwa ushauri inapotokea migongano ya kidini, kisiasa na utamaduni. Pale vijana wa CCM na hata Chadema walipopandisha joto la kisiasa ni Kingunge aliyeaminiwa kuwatuliza. Kingunge alikuwa ni mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Tunasema alikuwa kiungo muhimu baina ya pande mbili za Muungano na daima aliwakumbusha vijana umuhimu wa kuulinda. Mchango wake kwa Tanzania ni mkubwa na kamwe hatupaswi kuusahau. Hakika Taifa limempoteza gwiji wa itikadi na siasa za Tanzania. Pia tunaishauri Serikali iangalie namna bora ya kumuenzi kwa vitendo. Sisi tunaamini kwamba pamoja na kwamba hatutamwona tena, lakini maneno na ushauri wake vitaendelea kuishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles