28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

USHIRIKIANO DHAIFU BONGO MOVIE UTAIGHARIMU SANAA

NA MWANDISHI WETU

WAKATI mwigizaji wa sinema za Tanzania, Wastara Juma, akijiandaa kwa safari yake kwenda nchini India kupata matibabu ya mguu na mgongo, ni vyema tujadili ushirikiano dhaifu uliojitokeza kwenye sekta hii kipindi chote msanii huyo akiomba msaada.

Bila shaka nyakati za shida ndipo unaweza kubaini aina ya watu wanaokuzunguka, kama ni marafiki wa kweli au ni bandia wanaojali hali yako ikiwa timilifu.

Mpaka sasa ni kama mwezi mzima na siku kadhaa toka mwigizaji, Wastara aweke wazi matatizo yake na kuhitaji msaada wa matibabu ambapo ni wasanii wachache sana wa filamu walioonyesha kuguswa.

Mpaka Rais Dk. John Magufuli na mkewe mama Janeth Magufuli, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Bodi ya Filamu, walipoamua kuwa mstari wa mbele kuhakikisha msanii huyo anapata matibabu. Jambo lililoshangaza wengi ni ukimya wa wasanii wenzake ambao ni kama hawakuguswa na chochote.

Maswali yakatawala, watu wakajiuliza ina maana Wastara huwa hashiriki kwenye matatizo ya wenzake? Na kama huwa anashiriki kwenye matatizo ya wenzake iweje leo atengwe kiasi hiki.

Siwezi kumsemea Wastara ila kama kuna tatizo ndani yake basi ajitahidi kurekebisha maana wenzake waliibua hoja kibao zilizofanya mrembo huyo apoteze matumaini ya kupata matibabu.

Hata walipoibuka wadau wengine wa sanaa kama vile watangazaji wa vipindi vya runinga, baadhi ya wasanii wa filamu waliwatumia jumbe za kuacha kupaza sauti ya Wastara kwa madai kuwa akipata hiyo fedha huwa anaitumia kwa mambo yasiyofaa nje ya matibabu.

Taarifa hizo pia zilitufikia waandishi wa habari kutoka kwa baadhi ya wasanii wenzake wakitaka kuipotezea ishu ya Wastara na hapo ndipo nilipogundua ushirikiano dhaifu kwenye tasnia hiyo.

Na huenda vitu kama hivi ndivyo vikawa mwiba kwa ukuaji wa sekta ya filamu nchini. Maana kama leo mtu anaumwa na ana vielelezo vyote lakini bado wasanii wenzake wanampiga vijembe, je, wataweza kupeana michongo mikubwa ya kuinusuru sekta ya filamu?

Ni ndoto, hawawezi kusonga mbele na tutaendelea kuwa na waigizaji wengi wenye majina makubwa ambao hawana filamu kubwa, hili ni janga na endapo lisipofanyiwa kazi, tasnia hii itakufa kabisa, tuchukue hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles