30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WASIFU WA MWANASHERIA MKUU MPYA MZITO

NA EVANS MAGEGE

WAKATI Mwanasheria Mkuu wa Serikali mteule, Dk. Adelardus Kilangi, akitarajiwa kuapishwa leo Ikulu, jijini Dar es Salaam, wasifu wake unaonyesha ni mbobezi wa sheria za ngazi ya ndani na kimataifa, huku baadhi ya wadau wakimueleza kama mmoja wa watu makini.

Dk. Kilangi, ambaye anachukua nafasi ya George Masaju, aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahama Kuu, awali alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kituo cha Arusha.

Dk. Kilangi, naibu wake (DAG) atakuwa Paul Ngwembe, baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Gerson Mdemu, uteuzi wake kutenguliwa na kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Kabla ya uteuzi huo, Ngwembe alikuwa Mkurugenzi wa masuala ya sheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tanzania Insurance Regulatory Authority – TIRA).

Wasifu wa Dk. Kilangi

Wasifu wake uliochapwa kwenye mtandao wa Maktaba ya Umoja wa Mataifa (UN) ambao unahusu masuala ya sheria za kimataifa, unamtanabahisha Dk. Kilangi kama mbobezi wa sheria za kimataifa katika nyanja mbalimbali, zikiwamo sheria za madini na mafuta.

Dk. Kilangi, ambaye anatarajiwa kuapishwa leo Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, katika utendaji wake wa masuala ya sheria amewahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Afrika kati ya mwaka 2009 hadi 2015.

Akiwa mmoja wa wajumbe thabiti wa tume hiyo, aliteuliwa kuwa rais na akaiongoza tume hiyo kuanzia 2012 hadi 2014.

Dk. Kilangi amebobea katika Sheria za kimataifa za madini na katika utumishi wake amewahi kuwa Mkuu wa Idara ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino hapa nchini.

Pia amewahi kufundisha sheria katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Iringa), Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini – Dar es Salaam na Chuo Kikuu Huria.

Aidha, amewahi kuwa Meneja wa Mradi wa SAAT-Tanzania (Southern African Aids Trust) na Ofisa wa Mipango wa DANIDA na Mshauri wa Sheria wa Ubalozi wa Denmark hapa nchini.

Pia amewahi kufanya kazi kama Ofisa Mipango wa Mazingira, Haki za Binadamu na Jinsia katika asasi zisizo za kiserikali (NGO) na kuwa Mshauri wa Sheria wa Resource Mobilization Unit ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dk. Kilangi ni Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, pia ni mwanachama wa Chama cha Wanasheria cha Afrika Mashariki.

Ameandika vitabu na makala mbalimbali  kuhusu sheria, hususan eneo la sheria za ushirikiano wa kikanda, madini na sheria za kimataifa.

Amewahi kutoa ushauri na kufanya utafiti mahususi katika taasisi na mashirika ya maendeleo na maeneo ya mitaala na mipango ya maendeleo ya elimu.

Pia wasifu mfupi uliopo kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Linked in, mbali na uzoefu wake wa kazi, umetanabahisha kwamba, mwaka 2008 hadi 2013 alisoma Shahada ya Uzamivu wa Sheria ya Madini na Mafuta katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Pia alipata Shahada yake ya Uzamili, akibobea masomo ya usimamizi wa taasisi za kimataifa, biashara na uwekezaji.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi, anamtaja Dk. Kilangi kuwa ni mbobezi katika masuala ya sheria.

“Maoni yangu ni kuwa uteuzi wake naupongeza. Nadhani anayo sifa ya kuteuliwa kwa nafasi hiyo, kwa sababu ni mbobezi katika masuala ya sheria,” alisema Ngwilimi.

Naye Mratibu wa Mtandao wa Wapiganiaji wa Haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa, katika mazungumzo yake na gazeti hili, alisema kwamba, anamfahamu Dk. Kilangi kama mtu makini, mchapakazi na amewahi kufanya naye kazi nyingi kuhusu masuala ya haki za binadamu.

 

Inaendelea………… Jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles