31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KWAHERI JABALI

Na WAANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

KIFO cha jabali la siasa aliyefundisha maana halisi ya demokrasia na itikadi, Kingunge Ngombale Mwiru, kimeleta mshtuko kwa viongozi, wanasiasa, wasomi na watu wa kada mbalimbali.

Kijana huyo wa zamani wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye waliendesha pamoja harakati za kupigania ukombozi, alifariki jana saa 10:30 alfajiri, akiwa na umri wa miaka 85.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam, kwa takribani mwezi mmoja, baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake, Jijini Dar es Salaam Desemba 22, 2017.

Kifo chake kimekuja zikiwa zimepita siku 28 tu tangu afariki mkewe, Peras Kingunge, Januari 4, mwaka huu.

KAMATI YA MAZISHI

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi, Omary Kimbau, alisema Mzee Kingunge anatarajiwa kuzikwa Februari 5, mwaka huu, katika makaburi ya Kinondoni.

Akielezea namna kifo kilivyomfika mwanasiasa huyo mkongwe, Kimbau alisema baada ya kung’atwa na mbwa wake wiki tatu zilizopita, alikimbizwa Hospitali ya Kairuki, lakini baada ya muda waliamua kumhamishia Muhimbili Wodi ya Mwaisela.

“Alipofariki mkewe alikuwa amepata nafuu kidogo, hata madaktari walimruhusu kuja kumzika, lakini siku iliyofuata hali yake ilibadilika, ilibidi tumrudishe tena Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

“Kwa sababu ya umri wake, alipopata matatizo hayo, magonjwa mengine yalijitokeza, yakiwamo matatizo ya ugonjwa moyo, jambo lililosababisha kifo chake, lakini mpaka sasa hatujapata ripoti ya madaktari, ndiyo maana tunashindwa kusema chochote,” alisema Kimbau.

Alisema familia bado inaendelea na taratibu za mazishi ili aweze kuzikwa siku ya Jumatatu karibu na kaburi la mkewe, Pares.

Msemaji wa familia hiyo, Balozi Ali Mchumo, alizungumzia historia fupi ya marehemu Kingunge, akisema alibobea katika masuala ya siasa.

Alisema katika uhai wake, aliweza kukitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali katika idara mbalimbali.

Alisema mwaka 1950 marehemu alikuwa Katibu wa Chama cha Tanzania African National Union (Tanu) Rufiji, mkoani Pwani na ilipofika mwaka 1955 hadi 1957, alipelekwa na Serikali kusoma masuala ya Maendeleo ya Jamii na Siasa nchini Liberia na Senegal na alirudi mwaka 1968.

Aliporudi alichaguliwa na Serikali kuwa Mkuu wa Mikoa mbalimbali, ikiwamo Pwani, Mbeya na Tanga.

“Mwaka 1975 hadi 1995 alikuwa mbunge wa Kilwa na waziri kwenye wizara mbalimbali, ikiwamo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mpaka serikali inaingia kwenye mfumo wa vyama vingi,” alisema Balozi Mchumo.

Aliongeza, baada ya hapo, alichaguliwa kuwa mshauri wa Rais masuala ya Siasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kuanzia kipindi cha Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, hadi Rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete.

Balozi Mchumo alisema Kingunge pia aliwahi kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Marekebisho ya Katiba mwaka 2010, lililokuwa likiongozwa na marehemu Samuel Sitta.

Alisema katika Bunge hilo, Kingunge aliingia kama mlezi wa tiba asilia na hadi anafariki bado alikuwa mlezi wa Shirika la Tiba Asilia na Ulinzi wa Mazingira.

RAIS MAGUFULI: NIMEHUZUNIKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amesema amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha Mzee Kingunge, akimtaja kama mmoja wa waasisi wa Taifa hili na mwanasiasa mkongwe nchini.

Rais Magufuli, ambaye alimtembelea Kingunge Muhimbili takribani wiki tatu zilizopita, alisema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa TANU na baadaye CCM, na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.

“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wote, wanachama wa CCM, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu, na amewaombea kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

BUNGE LAMLILIA

Spika wa Bunge, Job Ndugai,  naye amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mzee Kingunge.

“Natoa pole kwa familia ya     marehemu na Watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza mwanasiasa mkongwe katika nchi hii ambaye licha ya kuwahi kuwa mbunge, lakini pia ameitumikia Serikali katika nyadhifa mbalimbali,” alisema.

Akimwelezea Kingunge, Spika Ndugai alisema yeye binafsi aliwahi kufanya naye kazi kwa karibu wakati wa Bunge na pia kwenye Bunge la Katiba, ambapo wote walikuwa kamati namba nane na yeye Mzee Kingunge akiwa Mwenyekiti wake.

Ndugai alisema wakati akiongoza kamati hiyo, mchango wake uliwasaidia sana.

Ndugai amemuomba Mungu awape subira, nguvu na faraja familia, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha kupotelewa na mpendwa wao.

HUYU NDIYE KINGUNGE

Kutokana na historia ya maisha yake, kazi na harakati alizozifanya kabla na baada ya ukombozi wa Taifa hili, jina lake lilitumiwa na baadhi kuelezea hadhi ya mtu.

Wanaomfahamu Kingunge wanamtaja kama Mjamaa kindakindaki, Mwanamajumui wa Afrika, Mzalendo halisi na mkweli.

Watu hao wanamwelezea Kingunge, ambaye amepata kufanya kazi kwa karibu na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kama ni miongoni mwa watu wachache walioshiriki katika ujenzi imara wa CCM.

Msingi wake ukiwa TANU, kama mwanachama kindakindaki na mpenzi wa mageuzi, akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana mwaka 1967/68,  wakati huo Joseph Nyerere alikuwa Katibu Mkuu na Moses Nnauye, ambaye ni baba wa Nape, akiwa Katibu Mkuu msaidizi.

Akipachikwa jina la utani la Susilov kutokana na kuvutiwa kwake na itikadi za Chama cha Kikomunisti cha nchini Urusi, Kingunge ndiye kiongozi wa mwanzo kuongoza Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, akishika nafasi ya Katibu.

Kingunge mwenyewe aliwahi kuliambia gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumapili katika  mahojiano maalumu Machi 17, 2017, kuwa yeye si tu mwasisi wa CCM, bali alikuwa kwenye jopo la watu 20 waliounda kamati ya kuandaa Rasimu ya Katiba ya CCM (1976-1977).

Wanaofahamu historia yake pia wanasema ndiye aliyeshiriki kuandika Azimio la Arusha kwa mkono wake mwenyewe.

Kumbukumbu zinaonyesha pia mwaka 1991, alichaguliwa na CCM kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kupendekeza Sera na Mwelekeo wa CCM.

Ripoti yake ndiyo inayotajwa  kujenga misingi ya mageuzi  ya uchumi.

Mwaka huo huo wa 1991, aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, kuwa mmoja wa wajumbe waliounda Tume ya Rais maarufu kama ‘Tume ya Nyalali’, kufanya utafiti na kupata majibu kuhusu matakwa ya Watanzania juu ya mfumo wa vyama vingi au chama kimoja.

Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo, Francis Nyalali, ilifanya kazi kwa mwaka mzima na Februari 1992, ilikabidhi ripoti yake kuhusu mtazamo na mapendekezo ya wananchi  ambapo mfumo wa vyama vingi ulikataliwa na Watanzania asilimia 80, huku 20 wakikubali.

SABABU ZA KUACHANA NA CCM

 

Inaendelea………. Jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles