26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

BITEKO AFUNGA MIGODI MAHENGE

Na MWANDISHI WETU – MOROGORO


NAIBU Waziri wa Madini, Dotto Biteko, ametoa siku tatu kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji madini katika migodi ya Epanko iliyopo Mahenge katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.

Biteko amechukua hatua hiyo baada ya ripoti ya timu maalumu aliyoiunda mwezi uliopita, kuonyesha hakuna usimamizi na udhibiti mzuri wa madini yanayochimbwa katika migodi hiyo na kuikosesha Serikali mapato.

Kutokana na hilo, Biteko aliiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Jacob Kassema, kuhakikisha ndani ya siku tatu shughuli zote katika migodi hiyo ziwe zimesitishwa hadi pale taratibu zote za kisheria zitakapofuatwa.

Pamoja na mambo mengine, Biteko alisema ndani ya muda huo wamiliki wote wa migodi hiyo wawe wameilipa Serikali hasara itakayobainika kutokana na biashara hiyo ya madini kufanyika kiholela.

“Tumekuja kuwaona mara ya pili, mnakumbuka tulitengeneza kamati ya kuja kupitia, baada ya kumaliza kupitia tumepata ripoti, tumeona mambo mengi hayaendi sawa, kwahiyo tumekuja kuchukua hatua.

“Muda mrefu sana mmekuwa hapa, lakini hatuoni mapato makubwa ambayo mnayapata ninyi yanayokuja serikalini ili yawanufaishe Watanzania.

“Uchimbaji wenu umekuwa hauzingatii sheria ya mazingira. Mapato mnayoyapata kama Serikali hatuyaoni, ili tuweze kujipanga vizuri, mjipange vizuri na Serikali ijipange vizuri, sisi tutafungua ofisi ya madini Mahenge ili ije kuwasimamia vizuri.

“Wakati tunakamilisha taratibu, lazima shughuli za hapa zisimame. Ninavyozungumza hapa kwa sababu mlianza kufanya kazi hamjapata ‘notice’, nawapeni siku tatu shughuli zote za hapa zisimame ili Serikali ijipange, iwasimamieni vizuri na mfuate sheria.

“Ndani ya siku tatu mfunge na Mkuu wa Wilaya chini ya usimamizi wako hakuna chombo hata kimoja kitakachotoka hapa mpaka tujiridhishe ni gharama kiasi gani imekwepwa na kiasi gani kinachotakiwa kulipwa.

“Halafu Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itaweka utaratibu wa kusimamiana, nimekuja kuwapeni taarifa wala hatuhitaji mjadala kwa leo, kwa sababu hali iliyopo hatuwezi kuvumilia upotevu wa madini na mapato uendelee kuwepo,” alisema Biteko.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji Tume ya Madini, Profesa Shukurani Manya, alisema ni kweli uchimbaji katika mgodi huo umekiuka taratibu nyingi za leseni.

“Tulipowapa leseni tulitegemea kabisa kwamba mtafanya kazi kwa masharti ya leseni, mnapaswa kujua kwamba baada ya kupewa leseni mitambo inapaswa ikaguliwe na maofisa madini ili wafanye utaratibu wa kuchenjua madini,” alisema Profesa Manya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles