25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 15, 2024

Contact us: [email protected]

Bilioni 988 kuboresha miundombinu Dar

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imesaini mkataba na Benki ya Dunia wenye thamani ya Euro milioni 361.1 sawa na takribani Sh 988.093 bilioni kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika leo Februari 20,2024 jijini Dar es Salaam kati ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu amesema mradi huo utaendelea kuboresha miundombinu muhimu ya umma katika Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni zilizokuwepo kwenye awamu ya kwanza.

Amesema mradi huo, sambamba na kupanua wigo wa uboreshaji miundombinu, wilaya za Ubungo na Kigamboni zimeingia katika mradi kwa mara ya kwanza.

Amesema lengo la mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM ya mwaka 2020 -2025)na ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kutanua na kuboresha miundombinu na huduma katika Jiji la Dar-es-Salaam.

“Hii ikijumuisha ujenzi na uboreshaji wa mtandao wa barabara katika kupunguza msongamano na kuimarisha mawasiliano, mitaro ya maji katika kupunguza athari za mafuriko pamoja na miundombinu ya masoko katika kutoa fursa za biashara na shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam”, amebainisha Dkt. Nchemba.

Amesema awamu ya pili ya mradi huo imezingatia ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi katika ujenzi wa miundombinu, miradi rafiki kwa mazingira na yenye lengo la kusaidia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naye Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, amesema wizara hiyo itasimamia kikamilifu mradi huo na kuhakikisha unatekelezwa kwa wakati.

Amesema mradi huo unalenga kujenga kimlomita 250 za barabara, kutokomeza changamoto ya taka ngumu, kujenga masoko ya kisasa 18, vituo vya mabasi tisa pamoja na mifereji mikubwa ya maji ya mvua ili kupunguza adha ya mafuriko jijini Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete amesema benki hiyo inajivunia kuwa sehemu ya ukuaji wa Dar es Salaam ambapo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita imetenga dola bilioni 1.5 kwa ajili ya ufadhili maendeleo ya jiji hilo.

Amesema mfano mzuri wa matokeo ya ushiriki wao katika maendeleo ya Dar es Salam unaonekana katika matokeo ya awamu ya kwanza ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam wa dola milioni 300 uliokamilika mwaka jana.

“Mradi huu ulijenga kilomita 207 za barabara na vituo vinne vya mabasi ambavyo vimeboresha usafiri kwa zaidi ya watu milioni 3.5 na kujenga kilomita 75 za mfumo wa maji na mabwawa matatu ya kuzuia mafuriko, kupunguza mafuriko kwa watu wanaoishi katika eneo la hekta 400 lenye hatari ya mafuriko,”amesema Belete.

Ameongeza kuwa mradi huo pia ulijenga masoko 10 na maeneo sita ya wazi ya wananchi kupumzika, kutoa fursa za kiuchumi na upatikanaji wa bidhaa na kufanya jiji kuwa mahali pazuri zaidi kuishi.

Belete amebainisha kuwa mradi huo pia ulianzisha mifumo ya kuongeza uwezo wa Serikali za Mitaa kuboresha ukusanyaji wa mapato, kutekeleza udhibiti wa maendeleo pamoja na kupanga na kudumisha miundombinu.

Akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Wabunge wa mkoa huo na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile, ameishukuru Serikali na Benki ya Dunia kwa kuwasikiliza na kutimiza ahadi yao ya hakikisha fedha hizo zinapatikana.

” Awamu ya pili ya mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa asilimia 70 ya mapato ya Serikali yanatoka jiji hili na asilimia 10 ya watanzania Dar es Salaam ni nyumbani, “amesema Dk. Ndugulile.

Ameomba mamlaka husika kuhakikisha mradi huo unaanza kwa haraka na kuahidi kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha unatekelezwa kwa wakati na unaendana na fedha zilizotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles