24.3 C
Dar es Salaam
Monday, September 16, 2024

Contact us: [email protected]

Bilioni 2.4 zatengwa kuboresha mawasiliano Geita

Na Yohana Paul, Geita

SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetoa kiasi cha Sh bilioni 2.42 kwa ajili ya ujenzi wa minara 17 kwenye maeneo yenye changamoto za mawasiliano mkoani Geita.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema hayo katika taarifa yake juu ya huduma ya mawasiliano mbele ya Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari alipokuwa ziarani mkoani Geita.

Justina amesema ujenzi wa minara hiyo ni sehemu ya mradi wa kitaifa wa ujenzi wa minara 758 nchi nzima ambapo kwa mkoa wa Geita mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha wananchi 242,000.

Amesema mradi huo unaenda kugusa kwenye kata 16 na vijiji 27 zenye changamoto kubwa zaidi ikiwa ni sehemu ya uboreshaji wa huduma ya mawasiliano kwenye maeneo yote nchini.

Amesema mradi huo umetanguliwa na mradi wa ujenzi wa minara 55 wenye thamani ya Sh bilioni 6.44 ambao upo mbioni kukamilika na tayari takribani watanzania 643,354 wamenufaika na mradi huo.

Amesema halmashauri tano mkoani Geita zimenufaika na mradi wa minara 55 ambapo Bukombe ilipata minara 10, Chato minara tisa, Mbogwe minara 18, Nyanghwale minara nane na Geita Dc minara 10.

Mbunge wa Jimbo la Busanda, Mhandisi Tumaini Magesa amekiri kabla ya mradi wa minara 55 jimbo lake lilikuwa na changamoto ya mawasiliano lakini sasa hali ni shwari na malalamiko yamepungua.

Mhandisi Magesa ameiomba serikali kuendelea kutatua changamoto za mawasiliano kulingana na ongezeko la watu ili Busanda iendane na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema mradi wa minara 17 utawanufaisha zaidi wachimbaji wadogo ambao wanafanya kazi maeneo ya milimani na wanapitia changamoto ya ukata mawasiliano.

Waziri mwenye dhamana, Nape Nnauye amesisitiza serikali kupitia TCRA na UCSAF imejipanga kuhakikisha inaboresha huduma ya mawasiliano na kusaidia wananchi wote kutumia mitandao kwa ufanisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles