Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WAKATI tukielekea katika msimu wa sikukuu, kasi ya upandaji bei za bidhaa za vyakula na nyingine, imeongezeka.
Takwimu zinaonyesha mfumuko wa bei wa taifa, mwezi Novemba, mwaka huu umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.5 ilivyokuwa Oktoba, mwaka huu.
Hii inamaanisha kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba, mwaka huu imeongezeka ikilinganishwa na kasi ya upandaji ilivyokuwa Oktoba, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Huduma za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo, alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari.
Kwesigabo alisema fahirisi za bei nazo zimeongezeka hadi 104.32 Novemba, mwaka huu kutoka 99.54 Novemba, mwaka jana.
Mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Novemba, mwaka huu umeongezeka hadi asilimia 6.2 kutoka asilimia 6.0 ilivyokuwa Oktoba, mwaka huu.
“Kuna vitu vingi vilivyochangia kupanda kwa mfumuko wa bei, ikiwamo bidhaa za vyakula, nyie ni mashahidi, mahindi yamepanda 15.6, samaki 23.7 nishati hasa mkaa umepanda hadi 22.1.
“Kundi la vinywaji na vilevi tumbaku zimepanda na gharama za afya na ukarabati nyumbani hasa vifaa vyake vimepanda kidogo,” alisema.
Alisema mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 1.1.
“Fahirisi za bei zimeongezeka hadi 104.32 Novemba, mwaka huu kutoka 103.17 ilivyokuwa Oktoba, mwaka huu. Kuongezeka kwa fahirisi hizo kumechangiwa na ongezeko kwa bei ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni mbogamboga kwa asilimia 7.4, unga wa ngano 2.4, unga wa muhogo asilimia 1.7, unga wa mahindi 1.5, mtama 1.5, dagaa wakavu 1.1 na mchele 1.0,” alisema.
Kwesigabo alisema kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi, ni pamoja na mafuta ya petroli kwa asilimia 1.4, mkaa 1.4, kuni 1.0, viatu vya watoto 0.7, mafuta ya taa 0.6, mavazi ya kike 0.5, mavazi ya kiume 0.4, mavazi ya watoto 0.4, viatu vya kike 0.3 na mafuta ya dizeli 0.2.
Alisema uwezo wa Sh 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa umefikia Sh 95.98 Novemba, mwaka huu ikilinganishwa na Sh 95.86 ilivyokuwa Oktoba, mwaka jana.