24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MO MFANYABIASHARA BORA AFRIKA 2016

mohammed-dewji-photograph
Mohammed Dewji

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

MFANYABIASHARA maarufu, Mohammed Dewji, ametangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Mfanyabiashara Bora wa Afrika wa mwaka 2016 jijini Paris, Ufaransa juzi.

Tuzo hiyo imetolewa na Vuguvugu la Ujasiriamali la Ufaransa (MEDEF), ambalo liliandaa jukwaa la kwanza la vijana na ujasiriamali Afrika kwa kushirikiana na Taasisi ya Choiseul.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana na ofisi ya Dewji, ilisema jukwaa hilo lilimpa tuzo mfanyabiashara huyo kwa kuheshimu mchango wake wa kuleta mabadiliko chanya katika kuendesha biashara, ambayo ni mfano kwa maendeleo na mafanikio ya Afrika katika kizazi cha sasa.

Ikiwa imeanzishwa mwaka 1988, MEDEF ni shirikisho mwajiri mkubwa zaidi nchini Ufaransa, likiwa na wanachama kama vile kampuni kubwa za Total, BNP Paribas, AXA Group, Micheln na L’Oreal.

Dewji, maarufu Mo, ambaye ni Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za MeTL, alizungumza kwa kirefu namna alivyopanga kusaidia mahitaji ya bara la Afrika kupitia maendeleo yanayochagizwa na sekta binafsi.

“Maendeleo endelevu ya kipindi kirefu ni kile kitakachoifanya sekta binafsi kushamiri barani Afrika.

“Na ili litokee, kampuni binafsi zinahitaji kuanza kuhusisha masikini kama wazalishaji, wasambazaji, waajiriwa na watumiaji sawa na namna MeTL Group inavyofanya nchini Tanzania,” alisema.

Mo aliitaka Ufaransa kuanza kuyatazama kwa mtazamo wa usawa mataifa yasiyozungumza Kifaransa kama ya Afrika Mashariki katika uwekezaji kutokana na ukuaji wa haraka wa uchumi na utulivu wa kisiasa eneo hilo.

Alimsifu Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa vita yake dhidi ya ufisadi, matumizi mabaya ya fedha, mali za umma na kuwa na maoni, ambayo yana msaada mkubwa kwa Afrika.

Alisema Serikali ya Tanzania ni mfano mzuri wa nyakati mpya za kufanya kazi kwa vitendo na ufanisi kwa maendeleo.

Akipokea tuzo hiyo, Dewji alitoa wito kwa vijana wa Afrika, ambao anaamini ni ‘alama ya matumaini.’

Alitoa nasaha kuwataka wasipoteze matumaini, bali waruhusu uwezo wao wa kiubunifu kuchochea mageuzi katika safari yao kama mawakala wa mabadiliko barani Afrika.

“Tunaweza kuweka mustakabali mpya uliojengwa katika ufahamu, kwamba mtangamano wa kiulimwengu ni msingi mkuu wa ustawi duniani,” alisema Dewji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles