Na ESTHER MBUSSI-NYASA
BIASHARA ya usafirishaji shehena ya makaa ya mawe inatarajiwa kushamiri katika Ziwa Nyasa na nchi jirani ikiwamo Malawi baada ya kukamilika kwa upanuzi wa Bandari za Kiwira mkoani Mbeya na Bandari ya Ndumbi iliyoko wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Ujenzi huo unaoenda sambamba na ujenzi wa meli mbili za mizigo za MV Ruvuma na MV Njombe zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kwa wakati mmoja kila moja, unaosimamiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), licha ya kurahisisha usafiri wa mizigo katika ziwa hilo, pia utachangia kuongeza shehena inayohudumiwa katika bandari za ziwa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abeid Gallus alisema lengo la mradi huo ni kupanua eneo la kuhifadhi shehena hususani makaa ya mawe ambayo yatakuwa yakisafirishwa kwa wingi hadi Bandari ya Kiwira na kuchukuliwa na malori kusambazwa kwa wateja.
“Shehena kuu katika bandari za Ziwa Nyasa ni makaa ya mawe ambayo hupitia katika Bandari ya Ndumbi iliyoko wilayani Nyasa hadi Kiwira na baadaye kusafirishwa na malori katika viwanda vilivyopo Mbeya.
“Aidha shehena ya makaa ya mawe pia husafirishwa kwenda katika bandari zilizopo nchi jirani ya Malawi kwa ajili ya matumizi katika viwanda nchini humo, lakini pia shehena nyingine zinazopita katika bandari za Ziwa Nyasa ni saruji, mabati, dagaa na mizigo mchanganyiko,” alisema.
Aidha, akizungumza meli hizo mbili za mizigo, Gallus alisema zinatarajiwa kupunguza idadi kubwa ya malori yanayopita barabarani kwa kuwa mzigo mwingi utakuwa ukipitishwa kwa njia ya maji na pia itaipunguzia Serikali gharama za ukarabati wa mara kwa mara wa barabara.
Alisema kwa mfano meli moja yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo ni sawa na malori 33 yenye uwezo wa kubeba tani 30 kila moja.
Naye mhandisi wa bandari za Ziwa Nyasa, Khamisi Nyembo, alisema meli hizo zikianza kazi zitafanya safari nne kwa mwezi, usafiri ambao utarahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka Bandari ya Ndumbi hadi Kiwira.
Kwa upande wake, mmiliki wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Liweta, uliopo Kijiji cha Liweta, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Richard Mahundi, alisema changamoto iliyopo katika usafirishaji wa makaa hayo ni miundombinu kwani barabara bado ni mbovu, lakini kwa sasa inaenda kuondolewa na usafiri wa meli hizo.
“Kwa sasa tunasafirisha tani 5,000 kwa mwezi, lakini meli itaturahisishia kubeba walau tani 2,000 kwa wiki na mteja wetu mkubwa ni Kiwanda cha Saruji Mbeya (Mbeya Cement).
“Pamoja na hayo tunamuomba waziri mwenye dhamana atuangalie kwa jicho la tatu wachimbaji wazawa kwa sababu wazawa bado hatujapewa nafasi kama Rais John Magufuli alivyodhamiria kuwainua wachimbaji wadogo wazawa,” alisema Mahundi.