RENATHA KIPAKA-BUKOBA
KAIMU Balozi wa Marekani nchini, Dk. Inmi Patterson, ametembelea miradi ya maendeleo mkoani hapa katika upande wa afya na kuutaka uongozi wa mkoa kufanya jitihada za kuondoa udumavu.
Akiwa mkoani hapa kwa ziara ya siku tatu, Dk. Patterson alisema lengo ni kufika katika miradi iliyofadhiliwa na Marekani kwani mkoa umekuwa ukifanya vizuri katika upimaji wa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) hasa kwa wanaume.
Hata hivyo Dk. Patterson alisema wananchi wamehamasika kupima katika vituo vya afya na utumiaji wa dawa za kufubaza nguvu za virusi.
“Nimefurahi kufika hapa na kujionea miradi tunayoifadhili, kikubwa ni kuona maambukizi ya VVU na nashuja zaidi,” alisema Dk. Patterson.
Katika hatua nyingine, alisema licha ya kuwa na chakula cha kutosha, bado hali ya udumavu ni kubwa, lazima uongozi wa mkoa uchukue hatua kulingana na takwimu za sasa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk. Marco Mbata alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa na kufanikisha kupunguza asilimia zilikuwepo kutoka 41.7 hadi 39.8.
Alisema elimu iliyotolewa juu ya matumizi bora ya lishe yenye kutumia chakula aina mbalimbali kuondokana na mlo mmoja wa ndizi kutwa nzima ilizaa matunda.
Naye Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisema kwenye mkoa huo kuna fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo kilimo, ufugaji na utalii.