Asha Bani-Dar es salaam
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limewataka watanzania kudumisha amani, upendo na kuvumiliana ili taifa liweze kusonga mbele.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Baraza la Ulaa na Naibu Kadhi wa Bakwata, Sheikh Ali Mkoyogole, wakati wa dua ya kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu 1441 Hijiria, iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Al haramain.
Alisema katika mwaka huu mpya wa Kiislamu kuna mambo mbalimbali ambayo Waislamu na watanzania kwa ujumla wanatakiwa kuyaenzi na kuyaendeleza ikiwa ni pamoja na upendo,amani,kushirikiana, kuvumiliana na kusamehe ili kuwepo na maendeleo baina ya waislamu na taifa kwa ujumla.
“Katika mwaka huu mpya wa kiislamu ujumbe wetu mkubwa ni Upendo na amani na endapo kutakuwa na vitu hivi basi kila kitu kitakwenda vizuri, na ikumbukwe kuwa vitu hivyo vinakwenda sambamba na kuvumiliana na kusameheana kwa wanadamu,’’ alisema Sheikh Mkoyogole
Aliongeza kuwa kama muislamu atakuwa hana upendo hawezi kumvumilia mwenzake wala kumsamehe hawezi kuweka amani lazima kutakuwa na machafuko ambayo hayatojenga.
Alisema huwezi kuwa katika nchi iliyokosa amani na upendo, watoto wakaenda shule, kazini na kufanya shughuli zingine za uzalishaji ni lazima kutayumba.
Alisema Watanzania wanatakiwa kuomba na kuwajalia viongozi wa taifa hili ujasiri ili waweze kuliongoza vyema taifa lenye maendeleo.
Naye Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Issa Athuman alisema katika mwaka huu mpya ni lazima waislamu wajipange katika kuondosha changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuweza kufikia malengo yao kwa mafanikio.
Mjumbe mwingine Sheikh Adam Mwinyi alisema katika kipindi hiki cha mwaka mpya Waislamu wanatakiwa kuendeleza orodha ya nini kinatakiwa kufanyika sambamba na orodha hiyo kuwa na mambo ya heri tupu.
Sherehe za kuukaribisha mwaka huo mpya wa Kiislamu zilihudhuriwa pia na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber na masheikh wa wilaya mbalimbali nchini.