28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NBS, wadau kuchunguza sababu za umaskini

Mwandishi wetu -Dodoma

BAADA ya kuzinduliwa kwa ripoti ya Matokeo ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Mwaka 2017/2018, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina mpango wa kushirikiana na taasisi za kitafiti kuchunguza sababu za hali ya umasikini katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa maendeleo kuhusu umaskini jijini Dodoma jana, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa, alisema ripoti iliyotolewa inaonesha picha ya umasikini ilivyo bila ya uchambuzi unaoonesha sababu za hali kuwa hivyo.

“Tuna mpango wa kushirikiana na taasisi za kitafiti nchini kama REPOA kuangalia sababu za hali ya umasikini katika katika ngazi za chini ili kujifunza kama ambavyo tulivyowahi kufanya huko nyuma,”alisema Mtakwimu Mkuu.

Kwa mujibu wa Utafiti huo, umasikini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011-12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017-18 huku umasikini wa chakula ukionesha kupungua kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.0 katika kipindi hicho hicho.

Katika mkutano huo wajumbe walipokea na kujadili ripoti hiyo ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi wa mwaka 2017/18 na maendeleo ya mfumo wa upimaji wa viashiria vya umasikini usiotokana na kipato pamoja na maendeleo ya maandalizi ya sensa ya kilimo ya mwaka 2019.

Mtakwimu Mkuu huyo wa Serikali  alisema kuwa mfumo wa upimaji wa viashiria vya umaskini usiotokana na kipato utawezesha kufahamu zaidi vyanzo vya umasikini na kusaidia kupanga mikikakati ya namna ya kukabiliana nao.

Alisema kuwa mfumo huo utawasogeza karibu watunga sera na wafanya maamuzi pamoja katika kukabiliana na tatizo la umasikini nchini.

Kutokana na hali hiyo Dk. Chuwa, alisema kuwa ripoti kamili ya utafiti huo ambayo inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwaka huu itagusia baadhi ya sababu za tatizo la umasikini nchini.

Aliwaambia wajumbe kuwa mapambano dhidi ya umasikini si suala la siku moja hivyo hapana budi kujivunia kiwango hicho kilichofikiwa katika kupunguza tatizo hilo la umasikini nchini.

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa Sensa ya Kilimo ya mwaka 2019, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa, alieleza kuwa hadi sasa hatua za awali za maandalizi yanaendelea vyema kwa msaada wa Idara ya Kilimo ya Marekani ambayo imekuwa ikitoa misaada ya kifedha na kitaalamu.

Hata hivyo, alibanisha kuwa pamoja na dhamira ya Serikali “Sensa hiyo ni zoezi kubwa linalohitaji fedha na nyenzo nyingi ambapo Tanzania haiwezi kuikamilisha bila ya ushirikiano na washirika wake”

Dk. Chuwa alifafanua kuwa takwimu zitakazozalishwa katika Sensa hiyo zitasaidia kufuatilia viashiria vya malengo ya maendeleo endelevu hususan lengo namba mbili pamoja na viashiria vya mipango ya maendeleo ya taifa.

“Kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, kufahamu hali halisi ya sekta hii ni muhimu ili kuweza kuchukua hatua stahiki na hilo linawezekana kwa kufanya Sensa kama hii,” alisema Dk. Chuwa

Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini, Betty Talbert, ambaye aliongoza kikao hicho aliwaeleza wajumbe kuwa pamoja na kuwa kazi ya kutayarisha ripoti hiyo iko katika hatua nzuri lakini alihimiza wajumbe kushirikiana na NBS kufanya uchambuzi kanzidata ya utafiti huo.

“Kanzidata ya utafiti huu ina utajiri mkubwa wa taarifa za kitakwimu ambazo zikifanyiwa uchambuzi wa kina zitaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na wadau wengine hivyo shime jitokezeni kusaidia uchambuzi wa kazidata hiyo,” alisema Talbert

Alibainisha kuwa miongoni mwa taarifa ambazo zitatokana na kanzidata ya utafiti huo ni pamoja na ripoti ya umasikini wa watoto ambao itatolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalioshughulikia Watoto (UNICEF) na taarifa maalum kuhusu matumizi ya muda katika kazi zisizo na malipo ambayo itatolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake-UN Women.

Mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia aliipongeza NBS kwa kasi iliyoonesha katika utayarishaji wa ripoti za utafiti huu na kwamba imekuwa ni mfano kwa wengine kuiga.

Wakati huo huo, Betty Talbert ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuisaidia Tanzania kufanikisha Sensa ya Kilimo ya mwaka 2019.

Talbert amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa wakati Benki ya Dunia inatambua mchango unaotolewa na wadau wa maendeleo kwa NBS kutekeleza Sensa hiyo lakini bado kuna pengo kubwa la nyenzo za kuwezesha kufanikisha utekelezaji wake kamili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles