ASKOFU wa Kanisa la Katoliki jimbo la Bunda mkoani Mara, Mhashamu Renatus Nkwande amewaasa mapadre wasijinufaishe na fedha za mashoga   kutoka nchi za Ulaya katika kuhamasisha haki za mashoga nchini.
Badala yake aliwashauri  wajishughulishe na kazi ya kuwakomboa katika dhambi.
Askofu alisema hayo juzi katika ibada maalum ya kumpa daraja Takatifu la Upadre, Shemasi Proper Luhinda iliyofanyika katika viwanja vya Parokia ya Mtume Paulo mjini Bunda.
Alisema   ushoga umeanza kuonekana pia mkoani Mara.
Aliwataka mapadre hao kutekeleza kiapo chao cha utii mbele ya Kanisa  na kwa jamii nzima kwa kupiga vita ushoga na aina zote za dhuluma huku wakiwahubiri jamii kutunza sheria za nchi na maadili ya Kanisa la Katoliki.
Naye Mkurugenzi wa miito ya Kanisa hilo Jimbo la Bunda, Padre Paulo Kamuhabwa aliwataka vijana wa kanisa hilo kujiunga na wito wa upadre kwa kuachana na anasa za dunia ili waitumikie jamii popote duniani.
Akisoma kiapo cha utii, Padre huyo mpya aliahidi kutimiza wajibu wake na kuwa na utii na mwadilifu kwa
Askofu wa jimbo hilo, mapadre, watawa na waumini wote.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alilipongeza kanisa hilo kwa utaratibu uliowekwa wa kuwapata mapadre wema.
Alitoa wito kwa waumini wa kanisa hilo kumuunga mkono Rais Magufuli katika kupiga vita maovu   nchini.
Mwakilishi Msaidizi wa Baba Mtakatifu nchini Ufaransa, Padre
John Italuma, aliwataka watanzania kutunza amani iiyopo ili kuepuka ugaidi kama yanayotokea Ufaransa hivi  sasa kwa kuua watu wasiokuwa na hatia.
Padre Prosper Luhinda anakuwa wa kwanza kupata daraja Takatifu tangu Jimbo la Bunda lianzishwe miaka mitano iliyopita.