Mwandishi wetu – Serengeti
TANZANIA ni kitovu cha simba duniania baada ya
kuwa na simba kati ya silimia 40- 50 za simba duniani katika hifadhi za
Taifa.
Akizungumza jana kabla ya kuanza kwa zoezi la kuwahamisha simba 17 kutoka
ikolojia ya Serengeti mkoani Mara kwenda hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato
mkoani Geita, mtafiti wa simba kutoka Taasisi ya Utafiti wa wanyamapori nchini
(Tawiri), Dk. Dennis Ikunda alisema hali hiyo inatokana na jitihada
zinazozofanywa katika kuboresha uhifadhi endelevu nchini.
Alisema pia hao asilimia 50 ya simba wa Tanzania wanapatikana katika ikolojia
ya Serengeti na hivyo kusema mamlaka husika katika hifadhi hiyo imekuwa
ikijitajidi kuhakikisha kunakuwepo na uhifadhi endelevu katika eneo hilo.
Alisema kutokana na uhifadhi huo endelevu, wamegundua idadi ya simba
imeongezeka katika ikolojia ya Serengeti na hivyo kuwa kubwa zaidi ya uwezo
wake hali ambayo imekuwa ikisababisha simba kutoroka na kuingia katika makazi
ya watu kufanya uharibifu.
Alisema kutokana na ongzeko hilo mamlaka husika zimeamua kuwahamishia baadhi ya
simba katika hifadhi ya Taifa ya Burigi ambako kuna idadi ndogo ya wanyama hao.
Dk. Ikunda alisema kabla ya kuhamishiwa huko, simba hao walifungiwa katika boma
maalum kwa zaidi ya siku 20 lengo likiwa ni kuwafanya wazoee mazingira mapya
ambayo wataenda kuishi.
“Kwavile kule Burigi kwa mujibu wa utafiti chakula kikuu ni pundamilia,
baada ya kuwakamata tumekuwa tukiwapa nyama ya pundamilia ili wakifika kule
wasipate shida, wawe wamezoea kwahiyo hatuna wasiwasi tayari wameshazoea hali
hiyo” alisema mtafiti huyo.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa), Misana Mwishawa,
alisema lengo la simba hao kuhamishiwa katika hifadhi ya Burigi ni kutaka
kuboresha na kuimarisha utalii katika hifadhi hiyo na nchini kwa ujumla.
Alisema simba ni miongini mwa vivituo vikuu vya utalii nchini hivyo maamuzi ya
kuwahamishia katika hifadhi hiyo ambayo ina simba wachache yalilenga katika
kuboresha sekta ya utalii huku akifafanua kuwa suala la kuhamisha wanyama
kutika katika hifadhi moja kwenda nyingine ni la kawaida na hufanyika kutokana
na uhitaji.
Alisema kuwa kabla ya kuwahamisha lazima utafiti wa kitaalam unafanyika ili
kujiridhisha na kwamba kutokana na simba kuwa wengi maamuzi hayo yanalenga
kuhakikisha kuwa idadi ya simba inaendena na ukubwa wa mazingira katika
ikolojia ya Serengeti.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alisema sekta ya utalii ina mchango
mkubwa katika uchumi wa nchi hivyo ni vema ikafanywa kuwa endelevu na kusema
kuwa zoezi la kuwahamisha simba kutoka Serengeti kwenda Burigi ni moja ya
mkakati wa kuendeleza sekta hiyo.