24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi 1,700 wa Shule moja Mwanza wakaa chini kwa kukosa madawati

Benjamin Masese – Mwanza

WANAFUNZI zaidi 1,700 wa Shule ya Sekondari ya Igoma jijini Mwanza wanakaa chini wakati wa masomo kitendo kilichowalazimu walimu kuwafundisha kwa mafungu na nyakati tofauti huku Mkuu wa shule hiyo, Kisumo Malima, akidaiwa kufanya jambo hilo siri.

Hayo yalibainika jana katika ziara ya  Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, waliotembelea baadhi ya  shule.

Wakiwa katika Kata ya Kishili eneo la Shule ya Msingi Kishili ambako walikutana kama kituo cha kupokea taarifa zote, Mtendaji wa Kata hiyo, John Mwakalasya alisowasomea taarifa ya miradi inayoendelea katika shule  mbalimbali.

Mwakalasya alisema ndani ya Kata ya Kishili kuna shule za msingi nne ambazo ni Kishili, Bukaga, Kanindo na Bujingwa ambazo zote zina miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu na mingine huku akimuomba Kiomoni kutoa fedha za kuezeka kwa yale majengo yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kukamilika.

Alisema kwa upande wa shule za sekondari zipo mbili ambazo ni Fumagila  na Igoma zina miradi ya ujenzi ya vyumba vya madarasa.

Hata hivyo licha ya taarifa hiyo kupongezwa kutokana na jitihada za wananchi kujitolea kujenga misingi na maboma ya madarasa, haikuanisha changamoto zilizopo katika shule na miradi inayoendelea.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni alisema licha ya taarifa hiyo  kuwa nzuri  na ya kuvutia kwa namna ya viongozi wa kata wanavyoshirikiana na wananchi kutatua changamoto kwenye shule, lakini kuna jambo wamelificha  la wanafunzi zaidi ya 1,700 wa Shule ya Sekondari Igoma kukaa chini wakati wa masomo kutokana na kukosa madawati.

Kiomoni alimsimamisha Mkuu wa shule hiyo, Malima ili kukiri au kukana mbele yake  kama watoto 1,700 hawana madawati   ambapo alikiri.

“Taarifa yenu ni nzuri kweli kweli na inanihamasisha kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia pale mlipoishia, naweza kusema Kata hii inaweza kuwa ya kwanza au ya pili  ndani ya Jiji la Mwanza kwa namna mnavyojitolea kuchangia shughuli za maendeleo lakini taarifa yenu  mmenificha  kinachoendelea Igoma Sekondari.

“Pale kuna watoto 1,700 wanakaa chini, hawana madawati kweli si kweli? Mkuu yuko wapi naomba asimame na akiri au akane mbele yangu (anasimama na kukiri), taarifa zote ninazo sasa bila kusema hapa  hiyo changamoto itaishaje hapo kwako?” alihoji Kiomonio.

“Kwa kuwa mmeonekana kufanya vizuri  ndani ya kata hii basi na mimi nasema ninatoa Sh milioni 20 kwa ajili ya kutengeneza mawadawati mara moja ya Igoma sekondari, naomba wasaidizi wangu mlichukue hili na lifanyiwe kazi mara moja ili madawati yapatikane.

“Nawataka viongozi wa kata hii hakikisheni mnakamilisha maboma ya vyumba vya madarasa ili kwa upande wa Serikali tuweze kuezeka haraka maana tunajua wanafunzi wanapata shida sana wakati wa masomo.Kwa uoande wa Shule ya Msingi Kanindo  nimeona kuna misingi mitano naombeni mkamilishe maboma  haraka na kwa hatua ya awali natoa mifuko 20 ya saruji,”alisema Kiomoni.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Nyimbi alipongeza viongozi wa Serikali za mitaa na kata kwa namna wanavyosimamia shughuli za maendeleo na kuwataka  kutokata tamaa huku akiwatahadhirisha kuchukua hatua dhidi ya mvua zinazoemndelea kunyesha na kuleta maafha ndani ya jamii.

“Wakati tunakuja  hapa tumepata taarifa ya matukio ya watu wawili kufariki likiwamo la mtoto kutumbukia kwenye dimbwi la maji na kupoteza maisha, vile vile la mtu kujinyonga  ambapo Mkuu wa Polisi Nyamagana amefika eneo ya tukio, jambo la kusisitiza tuchukue hatua mapema dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha maana baadhi ya wananchi wamejenga mabondeni na maeneo hatarishi,”alisema.

Ziara ya Dk. Nyimbi na Kiomoni bado inaendelea katika kata  mbalimbali za Jiji la Mwanza kukagua shughuli mbalimbali maendeleo huku wakijikita kuwataka   viongozi wa kata na mitaa kuhamasisha wananchi kuchangia fedha kwa ajili ya kuondoa changamoto zilizopo maeneo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles