27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

ANACHOTUAMINISHA GUARDIOLA KIGUMU KUKIAMINI

NA BADI MCHOMOLO


Hakuna kinachoshindikana katika soka, ndio wataalamu wengi wanasema hivyo huku wakidai kuwa soka ni mchezo wa makosa, hivyo ukikosea mwenzako anatumia nafasi hiyo na kujitengenezea ushindi.

Katika matokeo wengi wanatumia makosa ya wapinzani, lakini timu ikiwa na wachezaji wengi bora ni ngumu kuyaona makosa ya mara kwa mara yakitokea, kikubwa ambacho kitakuwa kinaonekana ni ufundi wa hali ya juu kuanzia kwa makocha hadi wachezaji.

Wiki iliopita ilikuwa ngumu kwa mashabiki wengi wa soka duniani kuamini kama Manchester City ambao ni wababe wa soka la England msimu huu wataweza kupoteza mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool kwa idadi kubwa ya mabao 3-0.

Wapo walioamini kuwa Liverpool wangeweza kushinda lakini sio mabao hayo, lakini bao 1-0 au 2-1, ila sio 3-0, lakini bila ya kuamini dakika 90 zilimalizika huku Liverpool wakiwa kifua mbele kwa ushindi huo mkubwa.

Huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya kwanza kwenye michuano hiyo mikubwa barani Ulaya na wanatarajia kurudiana kesho kwenye uwanja wa Etihad, huku mshindi wa jumla ya mabao mengi anatarajia kuingia hatua ya nusu fainali.

Baada ya mchezo wa kwanza kumalizika wiki iliopita tayari idadi kubwa ya mashabiki inaamini kuwa safari ya Man City kwenye michuano hiyo imefikia mwisho, kwa kuwa imeshindwa imefungwa mabao mengi na imeshindwa kupata hata bao moja la ugenini.

Huku mashabiki wakiamini Man City ndio baasi tena, lakini kocha wa timu hiyo Pep Guardiola anatulazimisha tuamini bado safari yao haijafika mwisho.

Inashangaza kidogo! Lakini wapo wanaoamini kauli ya kocha huyo akishirikiana na beki wa kati wa timu hiyo Vincent Kompany, ambaye amesisitiza kuwa wanatarajia kuishangaza dunia kwa kuweza kuwasimamisha wapinzani hao na wao kuendelea na safari yao.

Bado tunarudi pale pale kwamba hakuna kinachoshindikana katika soka. Msimu uliopita Barcelona waliweza kutuaminisha kitu ambacho wengi tulikuwa hatuwezi kuamini baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-0 jijini Paris dhidi ya PSG kwenye mchezo wa kwanza kwa kuwania kuingia hatua ya robo fainali.

Mchezo wa pili wa marudiano Barcelona walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani Camp Noun a kuishangaza dunia kwa kuwafunga wapinzani hao mabao 6-1 na kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali, haikuwa kazi rahisi lakini ilibidi tuamini kile ambacho hatukukiamini mwanzo.

Sawa Guardiola anataka kufanya kama kile kilichofanywa na Barcelona mwaka jana? Ngumu kuamini kwa upande wangu hasa kutokana na ubora wa wapinzani wao, ninaamini lengo la Liverpool kwenye mchezo huo wa marudiano ni kuhakikisha wanatafuta bao na kulipata ili waweze kuwapa wakati mgumu wapinzani wao kusonga mbele.

Tunaamini Guardiola amekuja nchini England kwa ajili ya kulete mapinduzi ya soka na kuweka historia kama alivyofanya akiwa ndani ya Barcelona kuanzia miaka ile ya 2008 hadi 2012 na akiwa Bayern Munich kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 kabla ya kujiunga na Man City.

Katika mchezo huo wa kesho, Guardiola atahakikisha anatumia wachezaji wake wote bora ili kuhakikisha maneno yake yanabaki kuwa kweli kwa mashabiki wake kwa kuwa hakuna ambacho kitakuwa kinamsumbua kwenye kichwa chake kwa ajili ya michezo mingine.

Ubingwa wa Ligi Kuu nchini England ni wa kwake, hicho ndicho alichokuwa anakiangalia kuweka heshima nchini humo, hivyo kilichobaki ni kuhakikisha anatamba kwenye michuano hiyo barani Ulaya.

Nitakuwa mmoja kati ya watu ambao watakuwa wa mwisho kuamini kauli ya kocha huyo na nahodha wake baada ya kumalizika dakika 90 za mtanange huo kwenye uwanja wa nyumbani wa Etihad, wakifanikiwa kuwazuia washambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane, Mohamed Salah na Roberto Firmino, basi kocha huyo anaweza kuitwa mfalme wa soka la kisasa barani Ulaya, ngoja tusubiri kesho kuona usiku wa Ulaya utakuaje.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles