33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

AG atoa maagizo kwa taasisi za umma

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi, amezitaka taasisi za Serikali kuwasilisha taarifa zote za mashauri ya madai kwenye ofisi hiyo ili hatua stahiki  ziweze kuchukuliwa.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya taasisi za Serikali kuendesha kesi zake bila taarifa kuwasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali hali inayosababisha hasara ambayo ingeweza kuzuilika.

Agizo hilo aliitoa jana jijini hapa wakati akizungumza katika kikao kazi cha wakurugenzi wa sheria, wakuu wa vitengo vya huduma za kisheria kutoka katika wizara, mamlaka za tawala za Serikali za Mitaa na idara zinazojitegemea.

 “Hivyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetoa maelekezo kuwasilisha taarifa zote za mashauri ya madai kwenye ofisi hiyo ili hatua stahiki  ziweze kuchukuliwa,” alisema Profesa Kilangi.

Alisema katika kuhakikisha mawakili wote wa Serikali wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao, Wizara ya Katiba na Sheria imetoa kanuni za maadili kwa mawakili hao zitakazotoa miongozo na kuweka miiko ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na mavazi.

Profesa Kilangi alisema katika kuboresha utendaji wa mawakili hao, ofisi yake imeandaa miongozo ya kutunga sheria ndogo, upekuzi wa mikataba mbalimbali pamoja na majadiliano yote.

“Wizara ya Katiba na Sheria kupitia tangazo la Serikali namba 600/2019 imetoa kanuni za maadili kwa mawakili wa Serikali itakayosimamia utekelezaji wa mikataba na kutoa ushauri wa kisheria,” alisema.

Alisema katika kurahisisha uratibu wa mawakili wote wa Serikali, wizara hiyo imeanzisha umoja wa mawakili wa Serikali wote nchini.

Profesa Kilangi alisema kupitia umoja huo mawakili wote waliopo katika utumishi wa umma  na wanaotekeleza majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  watapata fursa ya kukutana na kujadili mambo yanayohusu taaluma yao.

“Katika kuboresha shughuli za Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imesajili jarida litakalochapisha masuala muhimu ya sheria yanayohusu mihimili ya dola.

“Lengo la jarida hilo ni kutoa fursa kwa mawakili wa Serikali kuchapisha makala mbalimbali zinazohusu mihimili ya dola,” alisema.

Profesa Kilangi alisema Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kurekebisha madaraja na miundombinu ya kiutumishi  kwa wanasheria wote nchini.

Alisema kuwa ofisi hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mfumo maalumu wa kielektroniki wa kuwasilisha taarifa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoka katika wizara na taasisi zote za Serikali.

“Mfumo huu utakapokamilika utatumika ipasavyo kupokea na kutuma taarifa mbalimbali  baina ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wizara na taasisi zake,” alisema.

Alisema kuwa kupitia mfumo huo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itaweza kutambua mahitaji ya aina ya mafunzo ili kuongeza uwezo na ubobezi wa mawakili wa Serikali katika maeneo mbalimbali.

“Elimu hiyo itatolewa kwa utaratibu ambao utaandaliwa, ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa taasisi ya mafunzo ya wanasheria wa Serikali kama ilivyo kwa Chuo cha Mahakama Lushoto (IJA),” alisema Profesa Kilangi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles