Rukwa yaongoza kwa umasikini wa mahitaji ya msingi

0
476

FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MKOA wa Rukwa umetajwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha umasikini wa mahitaji ya msingi ikilinganishwa na Dar es Salaam ambao unashika nafasi ya mwisho kwa kuwa na kiwango kidogo cha umasikini huo.

Kwa mujibu wa utafiti wa mapato na matumizi ya kaya (HBS) wa mwaka 2017/18, uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), asilimia 26.4 ya watu wa Tanzania Bara wana umasikini wa mahitaji ya msingi, huku maeneo ya vijijini yakiongoza kwa asilimia 31.3 ikilinganishwa na mijini asilimia 15.8.

Katika ripoti hiyo ya utafiti uliopewa jina la ‘Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi kwa Tanzania Bara, 2017/18’, Mkoa wa Rukwa umetajwa kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha umasikini wa mahitaji ya msingi ambacho ni asilimia 45.0, huku Dar es Salaam ukiwa na kiwango kidogo zaidi cha asilimia 8.0.

Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa asilimia 8.0 ya watu wa Tanzania Bara wanaishi katika umasikini wa chakula ambao ni mkubwa katika maeneo ya vijijini kwa asilimia 9.7 ikilinganishwa na maeneo ya mijini ambako ni asilimia 4.4.

Pamoja na kiwango hicho cha kitaifa, ripoti hiyo pia imeenda mbali zaidi kwa kugusa ngazi ya mkoa, ambapo umasikini wa chakula ni mkubwa zaidi katika Mkoa wa Rukwa ambao una asilimia 19.8 ikilinganishwa na Kilimanjaro ambao una asilimia 2.1.

“Wastani wa kina cha umasikini wa mahitaji ya msingi katikia ngazi ya kitaifa ni asilimia 6.2 na wa kina cha umasikini wa mahitaji ya chakula ni asilimia 1.4,” imebainisha ripoti hiyo.

Aidha ripoti hiyo imeelezea kipimo cha fahirisi ya pengo la umasikini ambacho kinaweza kusaidia maofisa mipango na wasimamiaji wa sera mbalimbali za kijamii kujua ni kiasi gani cha fedha kitaweza kuwatoa watu masikini katika hali hiyo ili wafikie mstari unaopima kiwango cha umasikini.

“Kiasi kinachohitajika hupatikana kwa kuzidisha pengo la umasikini nchini (0.062) na idadi ya watu waishio katika kaya binafsi 52,691,314 na kiwango cha mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi (Sh 49,320).

“Kwa mwaka 2017/18 kiasi cha Sh bilioni 161.1 kwa mwezi zitahitajika kuondoa umasikini wa mahitaji ya msingi kwa watu waishio chini ya mstari wa umasikini Tanzania bara na kuwaleta kwenye mstari wa umasikini wa mahitaji,” imeeleza ripoti hiyo.

Hata hivyo, ripoti hiyo imefafanua kuwa mgawanyo wa kina cha umasikini wa vijijini ambao ni asilimia 7.4 ni mkubwa kuliko wastani wa taifa ambao ni asilimia 6.2 na ni zaidi ya mara mbili ya ule wa mjini ambao ni asilimia 3.5.

“Lakini kina cha umasikini kitaifa kwa kuzingatia tofauti ya kipato ni asilimia 2.1 ambapo kwa maeneo ya vijijini ni asimilia 2.6 ambayo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na mijini ambako ni asilimia 1.2,” ilisema ripoti hiyo.

Katika hatua nyingine, ripoti hiyo imeeleza mwenendo wa umasikini, ambapo imebainisha kuwa umasikini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011-12 hadi kufikia asilimia 26.4 mwaka 2017-18, huku kiwango cha umasikini wa chakula kikipungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011-12 hadi kufikia asilimia 8.0 mwaka 2017-18.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here