ANDREW MSECHU – dar es salaam
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana Juni 9 na 10, imeazimia kulaani mauaji ya raia nchini Sudan, kuimarisha uhusiano na vyama vingine vya siasa nchini, kupigania tume huru ya uchaguzi, kuzungumzia hali ya uchumi na sekta binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Zitto alisema katika kikao hicho walikubaliana kutoa salamu za mshikamano kwa raia wa Sudan wanaopita kwenye wakati mgumu.
“Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imepitisha azimio la kuitaka Serikali ya Tanzania kulaani mauaji ya wananchi wa Sudan, pili kuunga mkono maamuzi ya Umoja wa Afrika na tatu kumhoji Balozi wa Sudan nchini Tanzania kuhusu mauaji ya raia,” alisema.
Akizungumzia kuimarisha ushirikiano na vyama vya upinzani nchini, Zitto alisema viongozi wakuu wa chama hicho watakuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na vyama vingine vya siasa katika kuilinda misingi ya kidemokrasia nchini.
Zitto alisema Kamati Kuu imeendelea kuwapongeza mwanaharakati Bob Chacha Wangwe na Wakili Fatma Karume kwa kusimamia vema kesi ambayo Mahakama Kuu ya Tanzania ilibatilisha vifungu kwenye sheria ya uchaguzi.