Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuzindua rasmi treni ya umeme ya SGR, Shirika la Reli nchini (TRC) limesema abiria 100,000 wamesafiri tangu ilipoanza kutoa huduma Julai 14 mwaka huu.
Rais Samia anatarajiwa kuzindua treni hiyo Agosti Mosi mwaka huu kushuhudia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa mwishoni mwa mwaka jana ambapo aliliagiza TRC kuhakikisha safari zinaanza Julai.
Akizungumza leo Julai 30,2024 Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, amesema wastani wa abiria 4,000 wanasafiri kwa wiki kwa treni ya Dar es Salaam – Morogoro wakati abiria 8,000 wanasafiri kwa treni ya Dar es Salaam – Dodoma.
“Tulianza na treni mbili za kushuka na mbili za kupanda za kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro lakini ikaonekana hazitoshi, kuanzia Ijumaa mpaka Jumatatu zinajaa sana tukaamua kuongeza, mahitaji yakiongezeka tutaongeza kwa sababu tuna mabehewa ya kutosha…tiketi za tarehe moja zimeshajaa kwa Dodoma,” amesema Kadogosa.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema wako mbioni kutangaza utaratibu na vigezo vitakavyoiwezesha sekta binafsi kushiriki katika uendeshaji wa miundombinu ya reli hiyo.
“Sheria inaruhusu kushirikiana na sekta binafsi hivyo, tutatangaza utaratibu maalumu, tutaeleza vigezo ambavyo tunahitaji kwa kila kitu, mfano vichwa hatutaruhusu tu mtu alete lazima wazingatie ‘standard’ zinazoendana na reli ya kisasa,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesema reli hiyo itachangia ongezeko la mapato ya serikali na maendeleo ya shughuli za kiuchumi kwa kutoa usafiri wa uhakika na wa haraka na kwamba sekta zitakazoguswa moja kwa moja ni biashara, utalii, viwanda, kilimo, uvuvi na ufugaji.
Aidha amesema reli hiyo itapunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kusafirisha tani 10,000 kwa wakati mmoja na hivi sasa kazi ya kuunganisha reli na bandari hiyo inaendelea.
Kulingana na Waziri Mbarawa, mpaka sasa ujenzi wa kilomita 722 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umegharimu Dola za Marekani bilioni 3.138 wakati ununuzi wa vitendea kazi kama vile vichwa, mabehewa na treni za kisasa umegharimu Sh trilioni 1.3.