24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mzimu wa wanafunzi kujinyonga watikisa Kyela

Na IBRAHIM YASSIN-KYELA

SAKATA la wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Kyela Mkoani Mbeya kujinyonga,limeendelea kuumiza vichwa vya viongozi baada ya wiki iliyopita Grace Gowele (15) wa kidato cha pili na mkazi wa kitongoji cha Roma kukutwa amekufa kwa kujinyonga kwa kamba.

Baada ya Grace, mwanafunzi mwingine wa kidato cha nne wa shule hiyo hiyo naye alikutwa amejinyonga hali ambayo imezua taharuki.

Grace anadaiwa kujinyonga kwa madai ya kuchoshwa na tabia ya baba yake kumcharaza viboko huku shuleni pia akipewa adhabu hiyo hiyo.

Baadhi ya wakazi wa kitongozi hicho waliozungumza na gazeti hili walidai kuwa baba wa mwanafunzi huyo alikuwa na tabia ya kumcharaza viboko mtoto wake akimtuhumu kujihusisha au hata akimkuta kasimama na wanafunzi wenzake wa kiume.

Akisimulia kwa masikitiko tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Roma,Michael Mwakibinga,alisema ilikuwa saa mbili na nusu usiku alipigiwa simu akielezwa kuwa mwanafunzi kajinyonga ndipo alipofika eneo la tukio.

Alisema baada ya kufika aliamuru baba adhibitiwe kwa kuwa alitajwa kusababisha  kifo cha mwanae na polisi walipofika baada ya kupewa taarifa wakakuta wananchi wameupeleka mwili wa mwanafunzi huyo hospitali.

Alisema Polisi walipofika waliona kipande cha kamba kipo juu ya dari na kingine kikiwa chini kwenye shingo ya mtoto na pembeni yake kikiwepo kisu na hivyo kumchukua baba huyo na kumweka rumande wakimchunguza kabla ya kumtoa.

Wakati polisi wakimwachia baba huyo baada ya majibu ya hospitali kuthibitisha kuwa amejinyonga hata hivyo mama yake Elisia Msilanga alisusa maziko kutokana na mazingira ya kifo cha mwanae.

Baada ya kifo hicho pia juzi kilitokea kifo kingine cha mwanafunzi, Olipa Ephrahim Mwamkonda (17) wa kidato cha nne na mkazi wa kitongoji cha Itunge Kati aliyekutwa amekufa kwa kujinyonga kwa khanga.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kujinyonga baada ya kutaka kujiandaa kwenda shuleni hali ambayo imezua taharuki kwa wakazi wa wilaya hiyo. 

Akisimulia mkasa huo baba mdogo wa mwanafunzi huyo,Mawazo Issaya,alisema alipigiwa simu saa 1:00 asubuhi na majirani baada ya simu ya kaka yake ambaye ni baba mzazi wa mtoto kuwa haipatikani.

Alisema baada ya kufika eneo la tukio alimkuta Mwenyekiti wa kitongoji akiwa na kaka yake huku taarifa hizo zikipelekwa polisi ambao nao walifika bila kuchelewa.

Alisema baba mzazi wa mwanafunzi huyo,anaishi kitongoji cha Kapwili huku mtoto akiishi na bibi yake aitwaye Olipa Mafupa eneo la Itunge Kati na kwamba hadi sasa wameshikwa na butwaa hawajuhi sababu ya mtoto wao kuchukua uamuzi huo wa kujinyonga kwa kuunganisha khanga mbili na kufunga juu ya dari huku akikanyaga kiti na kukiachia.

Mpoki Mwaipaja Mwenyekiti wa kijiji cha Itunge amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa baada ya kufika eneo la tukio na kujionea alipiga simu polisi ambao walifika na kufanya taratibu zao za kipolisi na baada ya hapo waliuchukua mwili na kuupeleka hospitali ambako ulihifadhiwa na kesho yake ndugu walikabidhiwa kwa ajili ya maziko.

George Mwakila mkazi wa Mbugani,alisema huenda mazingira ya ukali wa walimu katika shule hiyo,yanasababisha  watoto kuchukua maamuzi hayo.

“Kama wazazi ni wakali wana waadhibu watoto na pia wanapofika shule wanaambulia adhabu ya viboko hali hiyo inaweza kuwa sababu ya wanafunzi kuona ni mateso na kuchukua maamuzi hayo ya kujiua” alisema.

Mkuu wa shule hiyo, Rehema Mwaipaja alipofuatwa na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake hakuwepo na wasaidizi wake waligoma kuzungumza chochote kwa madai kuwa hawajapata kibali kutoka kwa Mkurugenzi ambaye ni mwajiri wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Ezekiel Magehema licha ya kuthibitisha uwepo wa tukio hilo,alisema matukio yote yametokea majumbani mwao na si shuleni,na kwamba kutokana na hali hiyo walikaa vikao na wazazi,bodi walimu na wanafunzi wenyeji chini ya Mkuu wa wilaya ambapo mawazo yaliyotolewa yanafanyiwa kazi kuondoa changamoto hiyo.

Alisema mbali na hilo Rais Dk. John Magufuli aliwapatia Sh milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, ambapo na wao kama halmashauri katika bajeti ijayo watatenga fedha kujenga mabweni zaidi ili wanafunzi wa kike waweze kukaa shuleni hali itakayoondoa matatizo hayo.

Alisema tuhuma nyingine zilizosemwa hasa za mkuu wa shule si za kweli.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, Claudia Kitta, alikiri kuwepo na tukio hilo na kusema kuwa limetokea baada ya mwanafunzi kuchukia baba yake kumuadhibu kwa matendo yake mabaya ya kujihusisha na wanaume hali ya kuwa yeye ni mwanafunzi.

Alisema mtoto tukio la pili lililotokea juzi la mwanafunzi wa kidato cha nne kujinyonga limewashangaza na kulazimika kukaa vikao mbalimbali kutafuta namna ya kupambana na hali hiyo na kwamba hata Mkuu wa Mkoa alifika kwa ajili ya jambo hilo ambalo alisema ana uhakika ndani ya muda mfupi watalipatia ufumbuzi na kuondoa sintofahamu hiyo.

Kitta ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kyela, alitumia muda huo kuwaasa wananchi hasa wanafunzi kuacha kujichukulia sheria mkononi ya kujitoa uhai akisema kuwa ni bora kama kuna matatizo ya kifamilia kuwashirikisha viongozi wa mtaa na wa dini ili suluhu ipatikane badala ya kuchukua maamuzi magumu kama hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles