BEIJING, CHINA
WIZARA ya Mambo ya Nje ya China imesema Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema hakuna ushahidi kwamba virusi vya corona ambavyo vimewaathiri zaidi ya watu milioni 2 duniani vilitengenezwa kwenye maabara.
Msemaji wa wizara hiyo, Zhao Lijian ameyasema hayo jana wakati akijibu swali kuhusu shutuma kwamba virusi vya corona vilianzia kwenye maabara katika jimbo la Wuhan nchini China, ambako janga hilo lilizuka kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka jana.
Zhao aliwaambia waandishi wa habari mjini Beijing kwamba maofisa wa WHO wamesema mara kadhaa kwamba hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa virusi vya corona vilitengenezwa kwenye maabara.
Rais wa Marekani, Donald Trump jana alisema kuwa Serikali yake inajaribu kutathmini iwapo virusi vya corona vimetokea kwenye maabara ya Wuhan.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alisema China inahitaji kujisafisha kuhusu kile wanachokijua.
Zhao hakuzungumzia moja kwa moja kauli ya Trump.