Na JANETH MUSHI-ARUSHA
MWANAFUNZI Anna Zambi (16), aliyepoteza wazazi wake na wadogo zake watatu siku chache kabla ya kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, amesema anatamani kuwa mwanasheria ili aweze kusaidia watu wa makundi mbalimbali ikiwemo wanaofungwa kwa kuonewa.
Anna aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Wasichana yaMother Teresa of Calcuta ya mkoani Kilimanjaro, amefaulu kwa kupata daraja la pili na pointi 20.
Akizungumza jana jijini Arusha na waandishi wa habari nyumbani kwa mama yake mdogo, Isabella Lyimo, alisema anamshukuru Mungu kwa matokeo aliyoyapata japo ndoto yake ilikuwa kupata daraja la kwanza.
“Nilikuwa na ndoto ya kufaulu vizuri zaidi na kupata daraja la kwanza ila nimepata la pili, namshukuru Mungu kwa matokeo haya. Wapo waliokuwa na matarajio ya kupata ufaulu mzuri ila wamekosa.
“Tulikuwa jikoni tunasaidiana na dada kupika chakula cha mchana, mama mdogo akanipigia simu akaniambia matokeo yametoka, akaniuliza namba ya mtihani akaniambia nimefaulu kwa kupata daraja la pili, nilifurahi sana,” alisema.
 MWANASHERIA
Akizungumzia ndoto zake za baadaye, alisema anatamani kuwa mwanasheria ili kusaidia watu ikiwamo wanaobambikiwa kesi.
Alisema anakumbuka enzi za uhai wa baba yake, aliwahi kuwa na kesi, hivyo na kuanzia hapo alitamani kuwa mwanasheria ili aweze kumtetea baba yake.
“Nilitamani kuwa mwanasheria, awali baba alikuwa ofisa rasilimali watu katika moja ya taasisi Chalinze, alipata kesi ikafunguliwa mahakamani na alivyokuwa akirudi nyumbani alikuwa akilalamika kuwa kosa analokabiliwa nalo si la kweli, kuna hela zilihamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Baba alikuwa akisema angekuwa anajua sheria yasingempata yanayompata wakati huo. Na alituambia tuwe wanasheria ili ikitokea amerudishwa mahakamani tumsaidie.
“Nakumbuka alipata kesi nikiwa darasa la saba, hukumu ilikuja kutoka kabla sijamaliza kidato cha nne na ndipo umauti ulipomkuta. Natamani kusaidia na wengine, kuna wanaofungwa kwa kuonewa,” alisema.
SHULE ANAYOTAMANI KUSOMA
Anna alisema anatamani kuendelea kidato cha tano na sita katika Shule ya Canossa iliyopo Dar ss Salaam.
“Natamani kuendelea kidato cha tano Shule ya Canossa kwani naamini ni shule nzuri kitaaluma, hivyo mwanafunzi anavyosoma pale anakuwa na uhakika wa kufaulu,” alisema.
Mwanafunzi huyo aliwaliza Watanzania baada ya vifo vya wazazi wake Lingston Zambi, Winifrida Lymo na ndugu zake Lulu, Grace na Andrew, Novemba 16, gari waliyokuwa wakisafiria kwenda kwenye mahafali yake ya kuhitimu kidato cha nne kutumbukia kwenye daraja lililokuwa limevunjika kutokana na mvua Handeni mkoani Tanga.
Anna hakutaarifiwa msiba huo hadi alipomaliza mitihani na kurudi nyumbani kwao Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juma lililopita na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), katika Shule ya Mother Teresa Of Calcuta aliyosoma Anna, wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 121.
Kati ya wanafunzi hao, waliopata daraja la kwanza ni 12, daraja la pili 44, daraja la tatu 41 na daraja la nne 24.