Mahakama yaeleza mafanikio ukarabati miundombinu yake kwa miaka minne

0
487
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(kulia) akizungumza jambo leo wakati wa uwasilishaji wa mfumo wa Maktaba Mtandao uliofanyika katika ofisi ya Jaji Mkuu, jijini Dar es Salaam.

Na Magreth Kinabo-Mahakama

MAHAKAMA ya Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, imekamilisha miradi 42 ya ujenzi na ukarabati wa majengo yake katika ngazi zote kuanzia mahakama kuu hadi mahakama za mwanzo.

Miradi hiyo imetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutatua changamoto ya upungufu na uchakavu wa majengo ya mahakama na kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Mathias Kabunduguru, alisema kutokana na kukamilika kwa miradi hiyo, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuzindua majengo ya mahakama za wilaya za Ruangwa na Kilwa.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa litazinduliwa Januari 14, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma atazindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kilwa Januari 15.

“Tunajenga majengo haya kwa kuzingatia teknolojia ya habari na mawasiliano ili kurahisisha shughuli za utoaji haki kwa wakati,” alisema Kabunduguru.

Alisema miradi ya ujenzi iliyokamilika inajumuisha majengo manne ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma na Musoma na kuanzisha huduma za Mahakama Kuu na kuyafanyia ukarabati mkubwa majengo ya Mahakama Kuu kanda za Mbeya na Tanga.

Aidha, Mahakama ya Tanzania imekamilisha ujenzi wa majengo matano ya Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Pwani, Manyara, Geita, Njombe na Simiyu.

Katika kipindi cha miaka minne Mahakama imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa majengo 16 ya mahakama za wilaya ambazo ni Bagamoyo, Kigamboni, Mkuranga, Ilala, Kibaha, Babati na Bariadi.

 Majengo mengine ni pamoja na mahakama za wilaya za Chato, Geita, Bukombe, Ruangwa, Kilwa Masoko, Bariadi, Kondoa, Longido, Chunya na Kasulu.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Mahakama za Mwanzo, Mahakama  imefanikiwa kujenga majengo mapya ya Mahakama  za Mwanzo Kawe (Dar es Salaam), Mkunya (Newala), Msanzi (Sumbawanga), Mtowisa (Sumbawanga), Uyole (Mbeya) na Ngerengere (Morogoro).

Alisema Mahakama imekamilisha miradi ya ujenzi wa majengo ya mahakama za mwanzo iliyokuwa imesimama katika maeneo ya Iguguno (Singida), Bereko (Kondoa), Wasso (Loliondo), Old Korogwe na Magoma (Korogwe). Maeneo mengine ni Mvomero (Morogoro), Karatu (Arusha), Robanda (Serengeti), Itinje (Simiyu), Totowe na Mlowo (Songwe).  

Mahakama inaendelea na ujenzi wa majengo ya mahakama za hakimu mkazi katika mikoa ya Katavi na Lindi pamoja na wahakama za wilaya za Rungwe, Kilindi, Sikonge, Wanging’ombe, Makete na Bunda.

Aidha ujenzi wa majengo ya mahakama za mwanzo Mtae (Tanga), Laela (Sumbawanga), Lugarawa (Ludewa), Mang’ula na Mlimba (Morogoro) unaendelea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here