Zaidi ya wapiga kura milioni 190 wa Indonesia leo wanateremka katika vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mkuu ambao unaonekana kama mtihani kwa demokrasia ya nchi.
Wagombea wawili wa urais wako na ajenda sawa lakini wakitofautiana katika aina ya uongozi. Uchaguzi wa mwaka huu ni mkubwa ukihusisha uchaguzi wa rais, bunge na serikali za mitaa. Jumla ya wagombea 245,000 wanashiriki katika jumla ya viti 20,000 kwenye mabunge ya mikoa na kitaifa.
Rais wa sasa Joko Widodo anayejulikana zaidi kama Jokowi anakabiliana na Jenerali wa zamani Prabowo Subianto. Jokowi alishinda uchaguzi wa 2014 kwa asilimia 53 ya kura na wakati wa kampeni zake ameahidi kuimarisha uchumi na miundombinu. Utafiti wa kura za maoni unaonyesha rais Jokowi anaongoza katika uchaguzi.