NA OSCAR ASSENGA, TANGA.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amesema Serikali inatumia zaidi ya Sh bilioni 56 kwa ajili ya kuagiza samaki kutoka nje ya nchi kutokana
na kuwapo vitendo vya uvuvi haramu vilivyochangia kuua masalia ya samaki.
Mpina alisema hayo juzi wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Tanga kwa lengo la kukutana na wavuvi kwenye Soko la Sahare Kasera, jijini Tanga na Moa wilayani Mkinga pamoja na kusikiliza kero
zinazowakabili.
Alisema kitendo cha Serikali kuagiza samaki kutoka nje ya nchi kinazua maswali mengi kutokana na kwamba nchi inayo maziwa, bahari kubwa, mito mingi mikubwa ambayo ingeweza kutosheleza mahitaji.
Ziara hiyo inatokana na wito wa viongozi waliotaka afike kwenye eneo hilo ili kuweza kubaini changamoto zinazowakabili wavuvi hao na kuona namna ya kuzipatia ufumbuzi wa kina.
“Niwaambie kwamba nyavu haramu zilizokamatwa kwenye ukanda wa bahari kuu ukizibadilisha ni zaidi ya kilomita 773 zimekamatwa zilizokuwa
zinavua kwa njia haramu, leo hii watu wanapovua kwa kutumia sumu samaki wanateketea, Watanzania wanapoteza maisha kutokana na uvuaji wa namna
hii na tusipojipanga vizuri kuzilinda rasilimali za bahari zitatoweka,” alisema Waziri Mpina.
Aidha, Mpina alisema haiwezekani Serikali ikaagiza samaki kutoka nje hata kwenye nchi ambazo hazina mabwawa wala mito na kuwataka wavuvi kubadilika na kuzilinda rasilimali.
“Lakini pia niwaambie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ipo pamoja na wananchi wake ndio maana leo hii waziri nimekuja hapa na watendaji wengine wa Serikali kuwasikiliza changamoto zenu pamoja na hayo
niwaambie mnapoona Serikali inachukua hatua kwa ajili ya rasilimali hizo mjue ni kwa ajili yenu.
“Wapo wavuvi wanavua kwa nyavu halali na wapo wengine wanavua kwa nyavu haramu, ukienda kuvua kwa mabomu na nyavu haramu ni hatari kubwa
kutokana na kuharibu mazalia ya samaki na viumbe vingine vilivyopo majini, lakini pia kuhatarisha afya za walaji kutokana na kwamba wanaweza kupata saratani,” alisema.
Awali akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Msaidizi Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi, Mchira Wamarwa, alisema uendelevu wa rasilimali za
Bahari ya Hindi unatishiwa kutokana na kuwapo uvuvi unaofanyika kinyume na sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni za mwaka 2009 pamoja
na sheria nyingine za nchi ikiwamo sheria za mazingira namba 20 ya mwaka 2004.
Wamarwa alisema uvuvi haramu unaofanyika kwenye Bahari ya Hindi ni matumizi ya zana haramu na mbinu haramu za uvuvi, matumizi ya milipuko, kuvua bila
leseni, matumizi ya nyavu zenye macho chini ya nchi tatu, vyavu za timber, nyavu za dagaa zenye macho chini ya milimita 10, uvuvi wa katubi, kutumia vyombo visivyosajiliwa na kuvua kwenye maeneo yasiyosajiliwa.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji, alisema katika jiji hilo kipo kiwanda kimoja kinachochakata samaki ambacho kinakabiliwa na changamoto ya kukosekana samaki wa kutosha na kusabababisha kufanya kazi mara moja kwa
wiki au wiki mbili.
Mayeji alisema changamoto nyingine inayowakabili ni
uwekezaji wa kiwanda na kusisitiza hivi sasa utafiti unafanyika kubaini kama wanaweza kupata samaki wa
kutosha.
Mkurugenzi huyo alisema samaki wanaopatikana kwa
sasa hawatoshelezi kwa ajili ya kuendesha kiwanda na ndio maana wawekezaji wanasita kuwekeza.