23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Mtambo wa kutambua majanga ya moto kununuliwa

Na AMINA OMARI- LUSHOTO

WAKALA wa Huduma ya Misitu nchini (TFS), unatarajia kununua mtambo maalumu wa kutoa taarifa za majanga ya moto pindi yanapotokea katika hifadhi zake za asili.

Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema hayo alipokuwa akieleza mikakati yao katika kudhibiti majanga ya moto yanayotokea katika hifadhi zake za Chome na Magamba zilizoko mkoani Tanga.

Silayo alisema kifaa hicho kinachotarajiwa kugharimu Sh milioni 780, kitafungwa katika makao makuu ya wakala na kusisitiza kitakuwa na uwezo wa kusimamia na kutoa taarifa za moto.

Alisema licha ya kuchukua juhudi mbalimbali ikiwamo kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hizo, lakini bado baadhi ya hifadhi zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya uchomaji moto wa mara kwa mara.

“Licha ya kununua kifaa hicho, lakini tumeanza mazungumzo na wenzetu wa Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya kuanza ushirikiano ili kudhibiti matukio hayo kwa kiasi kikubwa,” alisema mtendaji huyo.

Naye Mhifadhi Msitu wa Hifadhi ya Asili ya Magamba, Getruda Nganyagwa, alisema kuwapo kwa sheria wezeshi kutasaidia kukuza shughuli za utalii katika hifadhi za misitu ya asili.

Alisema kuwapo kwa miundombinu yenye ubora kama vile barabara kutarahisisha kufika kwa haraka katika maeneo ya hifadhi hizo tofauti na ilivyo sasa.

Mhifadhi wa Msitu wa Hifadhi Asilia ya Chome, Sosthenes Rwamugira, alisema hifadhi hizo ni muhimu kwa uhai wa viumbe hai.

“Hifadhi za asilia zinazo umuhimu mkubwa kitaifa na kimataifa kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa bioanuwai ambao hawapatikani kwingine duniani isipokuwa Tanzania pekee,” alisema Rwamugira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles