*Matokeo Halmashauri ya Chemba yafutwa baada ya uongozi wa Wilaya kushiriki kuiba mitihani, kuwaonyesha wanafunzi
*Shule nyingine nane za Dar es Salaa, Mwanza, Kondoa zafutiwa matokeo, walimu wao, wamiliki wa shule kikaaongoni
Na ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limefuta matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba katika shule zote za msingi za Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma pamoja na Shule za Hazina na New Hazina zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, kutokana na udanganyifu.
Zingine zilizofutiwa matokeo ni pamoja na Aniny Nndumi na Fountain of Joy zilizopo Ubungo jijini Dar es Salaam, Alliance, New Alliance, Kisiwani zote za Mwanza na Kondoa Integrity iliyopo Kondoa mkoani Dodoma.
Shule hizo zimefutiwa matokeo baada ya kubainika kuvujisha mtihani huo uliofanyika Septemba 5 na 6 ambapo sasa zitarudia mtihani huo Oktoba 8 na 9.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema uchunguzi katika uliofanywa waliofanya, walibaini kuwa baadhi ya walivujisha mtihani huo wakishirikiana na waratibu elimu wa maeneo husika.
“Kuhusu shule za Halmashauri ya Chemba, uongozi wa idara ya elimu wa halmashauri hiyo ulipanga kufanya udanganyifu kupitia kwa waratibu elimu kata, walimu wakuu na wasimamizi ili kuhakikisha kuwa wanainua ufaulu wa halmashauri hiyo.
“Uongozi wa elimu Chemba uliunda makundi ya WhatsApp yaliyojulikana kwa jina la Elimu Chemba, Sayansi na Hisabati na wasimamizi Elimu Chemba ambayo yaliwajumuisha pia waratibu elimu kata na baadhi ya walimu wakuu, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano baina yao.
“Katika kutekeleza azma yao, mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifunguliwa kabla ya wakati na kusambazwa kupitia makundi ya WhatsApp waliyokuwa wameyaunda.
“Uongozi wa idara ya elimu Halmashauri ya Chemba, ulishiriki kutoa maelekezo yaliyohakikisha kuwa maswali yanafanywa na majibu yanawafikia watahiniwa kwa wakati, waratibu elimu kata walitekeleza kazi ya usambazaji wa majibu kwa walimu wakuu na watahiniwa,” alisema Dk. Msonde.
Aliwataja walioshiriki katika udanganyifu huo kuwa ni pamoja na Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Chemba, Modest Tarimo, Ofisa Taaluma Chemba, Ally Akida, Mratibu Elimu Kata ya Farkwa, Mwalimu Noela Chambo.
Wengine ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugenika, Joseph Mvuna, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makamaka, David Chilunda na waratibu elimu wa kata wote na walimu wakuu ambao pia walibainika kuunganishiwa kwenye makundi ya WhatsApp.
Kwa upande wa Shule za Msingi Hazina na New Hazina, Dk. Msonde alisema Septemba 6 mara baada ya mtihani wa somo la sayansi kukamilika, ofisa wa Necta alibaini uwepo wa kipande cha karatasi chenye maswali ya somo hilo karibu na chumba kilichokuwa kikihifadhiwa mitihani.
“Uchunguzi ulifanywa na Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Necta, ambapo ilibaini mmiliki wa shule kwa kushirikiana na walimu wa shule ya Hazina na New Hazina, walitafuta mitihani na kuipata siku moja kabla ya tarehe ya kuanza mitihani na kuwaonyesha wanafunzi wote wa shule hizo.
Alisema walimu wa Shule ya Hazina walibainisha kuwa walitumiwa mitihani ya masomo yote kutoka kwa walimu wa Shule ya Msingi Alliance iliyoko Halmashauri ya Jiji la Mwanza na simu za walimu wa shule hizi zilibainika kutumiwa mitihani ya darasa la saba ya masomo yote.
Dk. Msonde alisema walimu wa Shule ya Msingi Alliance walipokamatwa na kuchunguzwa, walikuwa na mitihani hiyo kwenye simu zao huku wakibainisha kuwa walipewa na walimu wa shule ya Aniny Nndumi ya Ubungo.
Alisema Mwalimu wa Shule ya Anny Nndumi naye alikiri kutuma mitihani hiyo ambapo alibainisha kuwa na yeye alitumiwa na mwalimu wa shule ya Fountain of Joy iliyopo Ubungo.
Aidha, Dk. Msonde aliwataja walioshiriki udanganyifu katika shule za Hazina na New Hazina kuwa ni pamoja na walimu; Heche Bahanzika Mohamed, Mambo Bakari Iddi, Lawrence Jacob Ochieng na Musa Juma.
Kwa upande wa Shule ya Msingi Aniny Nndumi waliohusika na udanganyifu, Dk. Msonde aliwataja kuwa Justus Mapesa James na Kenedy Malogo.
Dk. Msonde aliwataja pia mwalimu Benson Beita na Benson Awolo wa Shule ya Msingi Alliance.
Kwa upande wa Shule ya Msingi Kisiwani iliyopo Mwanza, alisema Septemba 9 wakati mtihani wa Hisabati ulipokuwa unafanyika, Afisa Mfuatiliaji wa Necta aliwabaini kuwa watahiniwa wa kiume walikuwa na majibu ya somo hilo.
Alisema Ofisa huyo alibaini watahiniwa hao wa kiume wameandika majibu ya somo hilo kwenye mapaja huku wale wa kike wakiwa wameandika kwenye fulana (t’shirt) sehemu ya pindo.
“Baada ya watahiniwa kuhojiwa walimtaja Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mugeta Maega Obeid kuwa alikuwa akiwapatia majibu kabla ya mtihani kuanza kufanyika.
“Hivyo inaonyesha kuwa mwalimu Odeke Dominic wa shule hiyo alikuwa ameiba mtihani kabla ya siku ya mtihani,”alisema Dk. Msonde.
Akizungumzia Shule ya Msingi Kondoa Intergrity iliyopo katika Halmashauri ya Kondoa, alisema Septemba 6 Ofisa Mfuatiliaji wa Necta alimkamata mtahiniwa mmoja akiwa na majibu ya mtihani wa somo la Sayansi.
“Mtahiniwa alipohojiwa alibainisha kuwa watahiniwa wote walikuwa wanapewa majibu ya mtihani ya masomo yote na walimu wao kabla ya mtihani kuanza,”alisema.
Aliwataja waliohusika na udanganyifu huo kuwa ni walimu; Brigita Lazaro Njiku, Christofa Daniel Christian na Epiphania Barnabas Mmbando.
Wengine ni wasimamizi waliosimamia mtihani shule ya Intergrity ambao ni Mwalimu Mariam Mchana, Alapha Omari, Betrice Mollel na Omari Kwarai.
Dk. Msonde alisema walimu wote waliotajwa walikamatwa na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
MAAMUZI YA BARAZA
Dk. Msonde alisema baraza hilo katika mkutano wake maalumu wa 125, uliofanyika jana limepitia kwa kina taarifa ya uvujaji wa mitihani uliofanywa na baadhi ya watumishi waliopewa dhamana ya kulinda mitihani.
“Kutokana na hilo, Necta imefuta matokeo ya shule hizo, ambapo utarejewa Oktoba 8 na 9. Pia baraza limefuta vituo vya mitihani vya Shule za Msingi Hazina na New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy, Alliance, New Alliance na Kisiwani na Kondoa Intergrity hadi hapo baraza litakapojirisha kuwa havitakiuka tena kanuni za mitihani,”alisema.
Alisema tayari baraza limeziarifu mamlaka za ajira na usimamizi wa sheria kuwachukulia hatua kali watumishi wote na mtu yeyote aliyebainika kujihusisha na kuvujisha mtihani kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi na Sheria za nchi.
Alisema kwa kuwa vituo vinane vya mitihani vimefutwa, baraza pia limeidhinisha vituo mbadala vya mitihani vitakavyotumiwa na watahiniwa katika mtihani wa marudio wa Oktona 8 na 9.
Alisema mtihani huo marudio katika Shule za Hazina na New Hazina, kituo cha mtihani watakachofanyia ni Shule ya Msingi Oysterbay iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Shule ya Msingi Fountain of Joy na Aniny Nndumi, alisema mtihani wa marudio utafanyika Shule ya Msingi Mbezi, Shule ya Msingi Kisiwani iliyopo Mwanza utafanyika katika Shule ya Msingi Kakebe.
Kwa upande wa Shule ya Msingi Alliance na New Alliance, alisema utafanyika katika Shule ya Msingi Mahina jijini Mwanza, Shule ya Kondoa Intergrity utafanyika Shule ya Msingi Bicha mkoani Dodoma.
Alisema baraza linaendelea kuchunguza uwepo wa udanganyifu katika vituo mbalimbali vya mitihani na kwamba halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na udanganyifu wakati mitihani ilipokuwa ikifanyika.
Naye Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais (Tamisemi) anayeshughulikia sekta ya elimu, Tixon Nzunda akizungumza kwenye mkutano huo, alisema Serikali imetengua uteuzi wa maofisa elimu wa wilaya ya Chemba na Kondoa waliokuwa wakisimamia mitihani hiyo.