Na Lilian Justice, Morogoro
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro  limewakamata watuhumiwa tisa wakidaiwa kuiba   dizeli lita 570 mali ya kampuni zinazojenga reli ya mwendokasi (Standard Gauge), maeneo ya Ngerengere wilayani Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa, alisema  tukio hilo lilitokea   Julai 7 mwaka huu   jioni.
Alisema kutokana na  msako mkali wanaouendesha waliweza kuwakamata vijana tisa wakiwa na   dizeli lita 570 yakiwa kwenye madumu ya lita 20 na lita 40 .
Kamanda  alisema   mafuta hayo ni mali ya kampuni zinazojishughulika na ujenzi wa reli  ya mwendo kasi zilizopo Ngerengere.
Alisema     watuhumiwa wanaendelea kushikiliwa na  jeshi hilo litaendelea kuwabaini wote wanaohujumu ujenzi wa taifa.
Katika msako huo, polisipia  walikamata dawa za kulevya zinazodaiwa ni heroine  kete 47  na bangi puli 15 na misokoto 160.
Alisema tukio hilo lilitokea Julai 30   mchana  maeneo ya Manzese manispaa ya Morogoro ambako Anna Selestine (30) alikamatwa na  madawa hayo akiwa ameyahifadhi katika  kikopo cheusi.
Kamanda   alisema   uchunguzi unaendelea na hatua za kumfikisha mahakamani mtuhumiwa zinaendelea.