26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

FAIDA YA ASPIRIN KWA WAGONJWA WENYE PRESHA YA KUPANDA

MIONGONI mwa dawa ambazo zilikuwapo tangu enzi na enzi ni dawa aina ya Aspirin.

Dawa hii ina zaidi ya miaka 100 inatumika na imekuwa msaada mkubwa katika kuimarisha afya za wanadamu.

Jina la Aspirin ni la kibiashara, ambapo kwa kitaalamu dawa hii huitwa acetylsalicylic acid.

Inawezekana ukawa ni miongoni mwa watu waliowahi kutumia dawa hii, iwe kwa kuandikiwa na daktari au kununua mwenyewe katika duka la dawa pasipo kushauriwa na wataalamu wa afya.

Lakini, kwa matumizi yaliyozoeleka na watu wengi ni kuitumia dawa hii kwa malengo ya kuondoa maumivu ya kichwa na viungo vingine katika mwili.

Pia dawa hii imekuwa ikitumika katika kushusha homa na kusaidia eneo lenye jeraha au uvimbe liweze kurejea katika hali yake ya uzima na kuweza kufanya kazi kwa ubora zaidi.

Kwa kitaalamu matumizi hayo yamegawanywa katika sehemu tatu ambazo ni kuzuia maumivu (Anti pain or Analgesic), kushusha homa (Antipyretic) na tatu ni kusaidia katika uvimbe na majeraha (Anti inflammatory).

Pamoja na matumizi hayo, inazo sifa ambazo huiwezesha kuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa na watu walio katika hatari ya kupata shinikizo la damu au presha ya kupanda.

Miongoni mwa vitu ambavyo humfanya mtu apate presha ya kupanda ni pamoja na kuongezeka kwa ujazo wa damu mwilini, mishipa ya damu kuwa miembamba kutokana na mwili kuongezeka au kuta za mishipa ya damu kuwa na mafuta, uzito wa damu kuongezeka na sababu nyinginezo ikiwamo msongo wa mawazo.

Katika sababu tajwa hapo juu, zinazosababisha mtu kupata presha ya kupanda, Aspirin husaidia kuiwezesha damu isiwe nzito kwa kuzuia mgandamano wa seli katika damu (inhibits platelet aggregation). Endapo seli zitagandamana katika damu, zitaisababisha damu iwe nzito na hivyo kuifanya presha ipande. Aidha, kutokana na damu kugandamana kutasababisha hatari ya kutokea tatizo la kiharusi (stroke) na hivyo kuhatarisha zaidi uhai wa mgonjwa. Seli zilizogandamana zinaweza kusafiri na kukwama katika mirija ya damu na hivyo kuzuia sehemu nyingine katika mwili isipate mawasiliano pamoja na damu kwa ujumla.

Ili kuweza kuepukana na tatizo la presha ya kupanda pamoja na hatari ya kupata tatizo la kiharusi, ni vyema ukapima afya yako sasa. Kiasi au dose ya dawa ya aspirin ambayo itakufaa kutumia itafahamika mara baada ya kuonana na daktari na kukufanyia uchunguzi wa kutosha.

Pamoja na umuhimu wa dawa ya Aspirin kwa wagonjwa wenye presha ya kupanda, pia zipo tahadhari za kuchukua kabla ya kuitumia. Tahadhari hizo ni pamoja na:

Dawa hii haishauriwi kutumiwa na mtu ambaye anayo historia ya kutokwa na damu mara kwa mara, mtu mwenye aleji na mchanganyiko wa dawa hii, mtu aliye na vidonda vya tumbo, mtu anayetumia dawa za kuzuia seli za damu kugandamana.

Pia, sababu za kutotumia dawa hii itategemeana na namna uchunguzi wa daktari utakavyokuwa.

Katika kuzuia presha ya kupanda, tuendelee kuzingatia kanuni za afya zinavyotuelekeza. Pia matumizi salama ya dawa ya Aspirin husaidia katika kupambana na tatizo hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles