26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

ESTHER: MAJI YAMENISABABISHIA ULEMAVU

Na HADIJA MRUTU


“NILIZALIWA nikiwa mzima  wa afya kabisa, sikuwa na ulemavu wowote, lakini nilipofika darasa la tatu nilianza kuona tofauti kwenye miguu yangu, baada ya kupita muda kidogo ilianza kupinda hadi kufikia hatua ya kupishana.”
Ndivyo anavyoanza kusimulia hali ya maisha aliyo nayo mkazi wa Kijiji cha Mtakuja, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro,  Esther Marko(19).

Esther akizungumza kwa huzuni na mtu anayeonekana kukata tamaa, anasema alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na  miguu yake kupinda.
Anasema baada ya miguu yake kupatwa na matatizo ya kupinda, lakini wazazi wake hawakujua chanzo nini.

“Wazazi wangu hawakujua sababu ya miguu yangu kupinda, baada ya kupelekwa Hospitali ya Seliani mkoani Arusha ndipo nilipoambiwa imesababishwa na maji tuliyokuwa tunatumia,”anasema.
Anasema pamoja na tatizo hilo kugundulika, alipewa dawa za kumsaidia, lakini hazikumsaidia vizuri kutokana na kukabiliwa na maumivu makali wakati wa kwenda shule.

“Nilikuwa napata wakati mgumu mno wakati wa kwenda shule, nililazimika  kupumzika njiani kusubiri maumivu yapungue au hata wakati mwingine kushindwa kabisa kuhudhuria masomo.
“Nimesoma kwa shida, hadi nahitimu darasa la saba,kuna wakati ulifika nikashindwa kwenda shuleni kutokana na maumivu,”anasema Esther.

Baba mzazi wa Esther, Marko Maleeka anasema  walikuwa wakitumia maji ya kisima  ambayo anaamini ndiyo chanzo cha kumsababisha ulemavu kwa mwanawe.

Anasema  alilazimika kuacha shughuli zozote za kiuchumi, ikiwamo kilimo ili kumpeleka mwanawe Hospitali ya Seliani kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji ili miguu inyooke.

“Nilitumia zaidi ya Sh 600,000 ikiwa ni gharama zote za kuhakikisha mwanangu anapatiwa matibabu, nilikodi gari kutoka hapa kijijini hadi Arusha kwa ajili ya matibabu,”anasema.
Anasema  hivi sasa, mwanawe anajishughulisha na kilimo na biashara ndogondogo ili aweze kumudu  gharama za maisha.

Mkazi wa Kijiji cha Tindigani, Martha Saruni ambaye pia aliathirika na tatizo hilo anasema tatizo hilo ni kubwa na linahitaji ufumbuzi wa haraka.

Anasema kuna baadhi ya wazazi ambao wamejitahidi kutumia fedha kwa ajili ya kuwatibu watoto miguu yao, wengine wamebaki hivyo kutokana na kukosa  fedha.
Anasema ni watoto wengi wameathiriwa na tatizo la maji na kushindwa kujiunga na masomo ya msingi.
Anasema hata mwanae Daudi tayari miguu yake, imeashaanza kupinda na kupata maumivu wakati wa kwenda shuleni.

Naye Asia Ramathani, mama wa watoto watano anasema  mtoto wake wa kwanza
Rajabu ameathiriwa na tatizo la maji, baada ya kufika darasa la tatu miguu ilianza kupinda na kupishana kabisa.

Anasema watoto wengine wannne waliobaki hawajathiriwa na maji,licha ya kuendelea kutumia maji hayo ya kisima ambayo ndiyo yaliyopelekea mtoto wake wa kwanza kupinda miguu.

Kwa sasa, familia imelazimika kutenga bajeti kwa ajili ya kununua maji ya Rajabu pekee, ambayo yanafuatwa karibu na Uwanja wa Ndege wa  Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA)  ambapo ni  mbali zaidi ya kilomita 15 kutokana Kijiji cha Mtakuja.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtakuja, John Masunga anasema kuna mtaalamu kutoka nje ya nchi, hamkumbuki jina alikuja na kuchimba maji yanayotoka ardhini Shule ya Msingi Mtakuja na kusema hayafai kwa matumizi ya binadamu kwa sababu ya floride.

Akizungumzia hali hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, Dk. Andrewleon Quaker ambaye pia ni daktari bingwa wa meno, anasema madini ya fluoride yakizidi kiwango yanaathiri zaidi mifupa na kusababisha kuvunjika.

Anasema tiba ya mifupa ambayo imevunjika, ni kuwekewa hogo kwa ajili ya kuunga,kwani madini hayo yanasababisha mifupa kuchakaa na kukosa nguvu.
Anasema njia pekee ya kuepukana na tatizo hilo ni kuacha kutumia maji ambayo yamezidi kuwago cha madini hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles