Na MAREGESI PAUL-DODOMA
MARA nyingi wanasiasa hawataki kuzungumzia mambo wanayoamini yanaweza kuwaathiri katika uchaguzi.
Lakini, Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema) anasema amekuwa mstari wa mbele kukemea uvuvi haramu ingawa sehemu kubwa ya wapiga kura wake ni wavuvi katika Ziwa Viktoria.
“Ukerewe ni kisiwa ambacho kina visiwa vingine 37. Kwa hiyo, jimbo langu lina wavuvi wengi wakiwamo wavuvi haramu.
“Pamoja na kwamba baadhi ya wapiga kura wangu ni wavuvi, tangu nilipokuwa nikiomba kura wakati wa Uchaguzi Mkuu, nilikuwa nikiwaeleza madhara ya uvuvi haramu na nimekuwa nikiwaeleza wasinipigie simu ili nikawaokoe pindi watakapokamatwa na kwa sababu ya uvuvi huo.
“Msimamo wangu huo ni wa hatari kwa sababu unaweza ukakupotezea kura, lakini wananchi wameweza kunielewa,” alisema Mkundi.
Pamoja na msimamo huo, mbunge huyo ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, anasema samaki wamepungua katika Ziwa Viktoria kutokana na uvuvi huo wa kutumia makokoro, sumu, timba na njia nyingine.
Ili kukabiliana na uvuvi huo, Mkundi anasema Benki ya Wakulima, inatakiwa kuwakopesha fedha wavuvi ili wavue kisasa kwani bila kufanya hivyo, uvuvi haramu utaendelea kwa kuwa wengi wao hawana uwezo wa kununua zana za kisasa zinazotakiwa na Serikali.
Kuhusu sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003, Mkundi anasema inatakiwa kurekebishwa kwani inawataka wavuvi wa dagaa watumie nyavu za milimita nane hadi 10 kuvua dagaa wakati Ziwa Victoria halina dagaa wakubwa kama walioko Ziwa Tanganyika.
“Kwa hiyo, tumekuwa tukiwasiliana na Serikali juu ya jambo hilo na kwa bahati nzuri wamekubali kufanya utafiti ili wajiridhishe na hoja zetu kabla hawajairekebisha sheria hiyo,” anafafanua.
Pamoja na hayo, Mkundi anaonyesha kukerwa na majambazi wenye silaha ambao wamekuwa wakivamia wavuvi katika Ziwa Victoria na kusema vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Kutokana na hali hiyo, anasema kuna haja Serikali iimarishe ulinzi ili kuwanusuru wavuvi hao kwani baadhi wamekuwa wakipoteza maisha na wengine kupata vilema vya kudumu pamoja na kupoteza zana zao za uvuvi.
Sekta ya kilimo
Akizungumzia sekta hiyo, Mkundi anasema baadhi ya mazao jimboni Ukerewe, yameathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na kuwafanya wakulima wasifaidike na kilimo kutokana na wadudu waharibifu kushambulia mazao yao.
“Kwa mfano, kuna ugonjwa wa batobato unaharibu sana mihogo na pia mahindi yanashambuliwa na funza. Hata wanaolima machungwa, mananasi na wenye miti ya miembe, hawanufaiki nayo kwa sababu hakuna soko la uhakika.
“Kwa kulitambua hilo, nimekuwa nikiwasiliana na Serikali ili tuangalie namna ya kukabiliana na wadudu waharibifu na pia watusaidie kupata viwanda vidogo vidogo na kutusaidia mbegu mbadala ili matunda yawepo msimu mzima wa mwaka.
Pia, anasema njia pekee ya kukabiliana na uhaba wa chakula wilayani Ukerewe ni kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika baadhi ya maeneo likiwamo Bonde la Miyogwezi ambako Serikali imeshawekeza zaidi ya Sh. milioni 600.
Usafiri wa majini
Kwa kuwa jimbo hilo ni kisiwa, Mkundi anasema kuna baadhi ya maeneo hayana usafiri wa uhakika kutokana na jiografia yake. Hata hivyo, anasema ameshawasiliana na moja ya kampuni inayomiliki meli binafsi katika Ziwa Victoria ambao wamekubali kufanya utafiti wa kupeleka meli yao kutoka Mwanza hadi katika visiwa vingine vidogo vidogo jimboni humo.
Sekta ya umeme
Katika sekta hiyo, mbunge huyo anasema hadi kufikia mwaka 2020, jimbo lake litakuwa na umeme katika vijiji vyote 75 ingawa kwa sasa ni vijiji zaidi ya 40 vilivyo na umeme.
“Ninaamini katika hilo kwa sababu hadi sasa Kisiwa cha Ukara kimeanza kupata umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na huduma hiyo inaendelea kusambazwa katika visiwa na vijiji vingine hatua kwa hatua.
“Kwa hiyo, nawaomba wananchi waendelee kuniamini, waendelee kuiamini Chadema na Ukawa na uchaguzi wowote utakapofanyika, wawapigie kura wagombea wa upinzani kwa sababu ndiyo watakaowaletea maendeleo ya kweli,” anasema mbunge huyo.
Sekta ya maji
Kuhusu sekta hiyo, Mkundi anaonyesha kushangazwa na Kisiwa cha Ukerewe kukosa maji ya uhakika wakati kimezungukwa na maji. Hata hivyo, anasema anashauriana na Serikali ili ifufue miradi ya maji iliyoko Ihebo, Bwisha, Irugwa, Bukindo na Bugorora ili iweze kusaidia kupeleka maji kwa wananchi.
Pamoja na hayo, anasema katika jimbo hilo kuna miradi miwili ya maji mjini na vijijini ambapo mradi wa mjini umekamilika ingawa bado una changamoto za kupasuka kwa baadhi ya mabomba na ule wa vijijini wakandarasi walishindwa kuendelea na kazi baada ya kucheleweshewa malipo. Hata hivyo, anasema wakandarasi hao wamesharudi kazini baada ya kulipwa.
Sekta ya afya
Mkundi alisema kuna vituo vitatu vya afya katika Kijiji cha Muriti, Bwisha na Kagunguli pamoja na zahanati 29. Hata hivyo, anasema sekta hiyo inakabiliwa na uhaba wa watumishi na vitendea kazi.
“Changamoto hiyo nakabiliana nayo kwani siku si nyingi, Zahanati ya Nakatunguru, iko mbioni kuanza kazi na Kituo cha Afya Bwisha, kitaanza kufanya upasuaji kwa sababu fedha za kuboresha miundombinu zimepatikana. Ile Zahanati ya Irugwa nimeshawapa mifuko 100 ya saruji kupitia fedha za mfuko wa jimbo ili kukiboresha na naamini kitakuwa katika hali nzuri baada ya siku chache,” alisema
Sekta ya elimu
Akizungumzia sekta hiyo, alisema wakati anaingia madarakani, aliikuta ikiwa na changamoto nyingi na sasa anafanya kila analoweza kuzitatua.
“Kwa upande wa shule za msingi, wakati Chadema tunaanza kuongoza Halmashauri ya Ukerewe mwaka 2010, tulikuwa wa mwisho katika matokeo ya darasa la saba katika Mkoa wa Mwanza, lakini baada ya kuanza kazi usiku na mchana, tulipanda na mwishowe tukawa wa kwanza kimkoa.
“Lakini, baada ya CCM kuongoza tena halmashauri yetu tangu 2015 baada ya kupata madiwani 18 na Chadema saba, elimu imeshuka na tumekuwa wa mwisho tena mwaka jana kimkoa.
Kwa hiyo, hilo ni somo kwa wananchi na sasa wanajua ni chama gani kinachowafaa na ni chama gani kisichowafaa.
“Lakini, najitahidi kutatua changamoto hizo kupitia nguvu za wananchi na fedha za Mfuko wa Jimbo. Kwa mfano nimetoa Sh. milioni 11 katika Shule ya Msingi Malegea, Shule ya Msingi Chifule tumepeleka Sh. milioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa choo na Kata ya Nakatunguru tumewapa Sh. milioni 8 za vyoo na shule za msingi na Serema wamepewa Sh. milioni 11 kupitia Mfuko wa Jimbo.
“Kwa upande wa shule za sekondari, hali ni ile ile, tunashirikiana na wananchi pamoja na wadau mbalimbali na kutumia mfuko wa jimbo. Pamoja na hayo, tatizo kubwa linalotukabili sasa ni uhaba wa walimu, lakini Serikali imeahidi kunisaidia kulitatua,” alisema
Akizungumzia siasa alisema nafasi ya CCM kuendelea kubaki madarakani baada ya 2020 ni ndogo kwa sababu wananchi wamechoshwa na maisha magumu yanayowakabili.