DIASPORA TUNAYO NIDHAMU YA KUFANYA KAZI

0
527

UONGO ni kitu ambacho ni cha gharama sana kwa wale ambao wanasema uongo na wale ambao wanadanganywa. Mazingira haya yanaleta misingi isiyokuwa imara na ubovu huo utakuja kugharimu wahusika na jamii.


Wakati uongo unachukua nafasi ya ukweli na uwazi jamii inaoza na uhusiano kati ya wanajamii unakuwa wa mashaka na watu kutokuaminiana na ule mfumo wote wa uhusiano unatetereka katika jamii na kudhoofika.


Jinsi jamii inavyokuwa na msingi mzuri na jinsi matawi yanaimarika na hata kutoa matunda mazuri. Yote inaanza kwenye mizizi na ni rutuba gani inapewa. Umwagiliaji unaweza kuwa unatoka juu lakini hata chini kwa chini unawezekana. Tuwe waangalifu na makini wakati unajenga jamii ya kesho msingi mzuri unawekwa sasa hivi, dakika hizi za mapambazuko.


Maadili mazuri ambayo yanakaa muda mrefu ni yale ambayo yanaeleweka, ni yale ambayo mtu unayaelewa undani wake na sababu zake na ambayo unaweza kuyafanya yako. 
Usipoyaelewa kiundani mwake utawezaje kuyafanya yako? Ukimlisha mtu kwa nguvu kuna hatari akaja kutapika na akaja kukinai hicho chakula.  


Ni jambo jema tukiwa makini wakati jamii inaelimishwa kuhusu maadili ya kimaisha. Kama tunakosea kama viongozi kwenye jamii zetu ni kukubali na kukiri makosa yetu, hakuna mtu asiyekosea na ndio maana tunaitwa binadamu. Watoto wa Adamu. Na hata yeye alimkosea Mwenyezi Mungu. 


Viongozi wote wakubwa si wadogo lazima twende na mifano na wengine waige, kwani ukiwa kwenye jukwaa macho na masikio yote yapo kwako wajinga wataiga lakini werevu watakufuata na waelewa watakusikia na kuimarisha ngome zao kiweledi. Yule ambaye hakupi ukweli basi nia yake ni kukugawa msiwe na sauti moja  na kukutawala. 


Haya yote yanaleta ubovu wa msingi wenu na katika jamii yoyote ile. Baadhi ya imani za mwanadamu mara nyingi zinakufunga kwa sababu ni imani zinakufunga macho na kukuziba masikio. 


Unazidi kuwa mtumwa wa imani mbovu na ambazo hazina ukweli ndani yake. Moja ni kama kufikiria kwamba ulemavu wa ngozi unaleta mafanikio au utajiri kama si ni utumwa wa fikra mbovu basi mimi sijui  niseme nini. 


Habari kama hizi huingizwa katika imani ya mwanadamu na kusambazwa yote hayo ni mitego ya kukufanya wewe mtumwa. 
Huu wote ni uongo ambao hauna maendeleo katika jamii. Kujiepusha na uongo kama huo ni kuongeza ujuzi na ukweli katika jami zetu.

Kazi moja kubwa ya Wanadiaspora ni kuja na ujuzi na ukweli wa mambo ambayo yanaboresha  jamii zetu na kuimarisha misingi mizuri katka jamii. Katika kuimarisha ukweli na ujuzi misingi ya kuhakikisha kwamba ukweli na ujuzi utalindwa wakati wote. 


Ujuzi unaweza kuboreshwa na ukweli kurekebishwa kutokana na habari ambazo zinatokana na ujuzi uliopatikana kwa wakati huo. Yote ni kwa malengo ya kuwa na jamii ambayo inastawi na mavuno ni mema tu. 


Diaspora ni kundi au jamii ambayo inakuja na ujuzi mkubwa sana na kuziba pengo hilo wataweza  kuchangia mengi. Ni muhimu kuelewa kwamba hao hao Diaspora lazima wawe kitu kimoja na kuweza kupeleka nguvu zao kwa pamoja na jamii kufaidika. 


Ni hatari kama katika safari hiyo mizizi ya utengano inawekwa chini kwa chini, hili jambo lazima tuepukane nalo. Katika jami ya Diaspora bila ya kuona ukweli macho kwa macho tutapotea. Kuna mimea fulani ambayo haiwezi kuishi yenyewe bila ya kuota kwenye miti mingine, ina mifumo ya mizizi ambayo ipo mpaka kwenye shina, matawi au matawi ya mti wenyeji. 


Inatumia pia virutubisho vya mti mwenyeji pamoja na maji kwa ajili ya kuishi, na si nzuri kwa afya ya miti yako. Ni muhimu tuwe na ajenda ambayo ni ya wazi na tukikaribisha mawazo potofu na msimamo ambao hauna tija katika jumuiya ya Diaspora basi hiyo pia  itaathri uhai wa jumuiya yetu. 


Diaspora ikiwa imesimama imara na ina falsafa na fikra ambazo zinajenga na malengo yake ni kuwa na uwazi na kutokuwa na ajenda za chini chini. Madhara ya kutokuwa na huo msimamo ni kwamba, tunaweza kuathiri jumuiya ambayo tunataka kushirikiana nayo. 


Wakati nchi inatafuta wataalamu katika sekta tofauti hapa ni kuangalia katika hili kundi na kutengeneza mazingira chanya ambayo yatawawezesha diaspora kuingia katika mfumo wa uhakika ambao Utafungua mila ya wao kuweza kuchangia kikamilifu. Wajuzi wa ndani ya nchi na wajuzi wa nje ya nchi Watanzania na wazawa hii nchi itapiga hatua moja kubwa sana. 


Diaspora ikihofiwa kwa sababu ya habari ambazo si  za kweli na woga ambao hauna maana basi tutakosa kisima cha ujuzi na uelewa. Si jambo la ajabu kwa mwanadiaspora mmoja tu kuwekeza kwenye shilingi miioni 100 na zaidi, kifedha na hata kitaalamu na kiujuzi.


 Serikali inaweza pia kuuza hisa maalumu kwa wanadiaspora tu ambayo inaweza kurudishwa na baada  ya miaka kadha na  wote ni washindi. Tuseme ukweli Diaspora ni muhimu kwa nchi yetu, Diaspora wanahitajika.


Watu wengi wanayo picha ya Ughaibuni ni mahala pa starehe. Hapana, hapa ni mahali pa kufanya kazi kweli kweli. Bila ya kufanya kazi ni mahali pagumu. Hakuna shamba utakimbilia kulima..hakuna. Ukishafahamu haya yote Iliyobakia ni kukamilisha uliyoyapanga.


Tunakuja na nidhamu ya kufanya kazi na mapenzi kwa nchi yetu. Tunakuja na ujuzi na tunakuja na nia ya kuwekeza. Ombi letu tu ni mtuwekee mazingira ya kutuwezesha tushiriki kikamilifu. Mazingira ya kweli na sisi tuchangie kwenye kuimarisha huo msingi..
Ukishafahamu hilo ni kupanga tu na kutimiza malengo yako.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here