SEOUL, KOREA KUSINI
KOREA Kaskazini imerusha kombora la masafa marefu katika Bahari ya Japan, katika kile wachambuzi wanachokiita onyo kabla ya mkutano kati ya viongozi wa China na Marekani.
Wizara ya Usalama ya Korea Kusini imesema kombora hilo limerushwa kutoka umbali wa kilomita 60.
Korea Kusini imesema, tukio hilo linatishia amani na utulivu duniani kote.
Naye Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, amelaani vikali tukio hilo na kusema kuwa ni uchokozi mkubwa kutoka Korea Kaskazini.
“Ni uchokozi mbaya kwa usalama wetu wa nchi, na ni wazi unakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hili haliwezi kustahimilika. Nitaitisha mkutano na Baraza la Usalama la Taifa mara moja," alisema Shinzo Abe.
Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, alisema Marekani imeshasema vya kutosha juu ya Korea Kaskazini na sasa haina maneno zaidi.
Kufyatuliwa kwa kombora la masafa ya wastani la aina ya KN-15 kutachochea wasiwasi duniani kuhusu mpango wa silaha wa Korea Kaskazini.
Taifa hilo lina mpango wa kuunda kombora la masafa marefu lenye kichwa cha nyuklia, likiwa na uwezo wa kuruka hadi katika ardhi ya Marekani.
Korea Kaskazini tayari imeshafanya majaribio matano ya silaha za nyuklia, mawili kati yao yalifanywa mwaka jana.