27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

SABUKURU YA MARAIS INAFELISHA MAENDELEO AFRIKA?

Na Markus Mpangala,

WAPO watu wanaohusisha umasikini wa Bara la Afrika na umri wa watawala wanaotuongoza.  Tunaposema Sabukuru tuna maana ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa au kumtamkia mtu heri ya siku ya kuzaliwa (happy birthday).

Watu hao wanasema kuwa viongozi wengi wa bara hili wana umri mkubwa sana hivyo kuwa sababu ya kukosa maendeleo barani humu.

Wakosoaji wanadai umri wa watawala wa Ulaya na Amerika ni mzuri kuliko wa watawala wa Afrika. Eti umri wa Robert Mugabe ni mkubwa hivyo kuwa chanzo cha maisha duni ya Wazimbabwe. Wapo watawala mbalimbali wanaotajwa katika muktadha wa umri.

Inaelezwa kwamba, wastani wa umri wa watawala wa Afrika ni 75-6, hivyo basi viongozi wengi wa Bara la Afrika wanaingia madarakani wakiwa na umri wa miaka 76. Ili kujiridhisha kwa hoja zao wanasema umri wa watawala wa nchi za Magharibi una wastani wa miaka 51, hivyo kwa umri mkubwa viongozi wa nchi hizo huwa na miaka 51.

Kwa hiyo tofauti ya umri wa watawala wa Afrika na nchi za Magharibi ni  miaka 25. Je, tatizo la Afrika ni nini? Kujadili hilo lazima tuangalie kwa namna mbili; mosi, masuala ya ndani ya nchi za Bara la Afrika.

Pili; masuala ya nje ya Bara la Afrika. Mathalani uhusiano wake na mataifa mengine tangu kuwepo kwa nchi hizi. Suala la uchumi, siasa, jamii na kadhalika. Si jambo rahisi kutumia kigezo cha umri wa watawala kuwa sababu ya maendeleo hafifu yaliyomo barani Afrika.

Je, umri wa watawala wako hapo unaingia namna gani? Kwamba utumishi wa umma, wataalamu wa sekta mbalimbali ni wahanga wa umri wa rais wa nchi? Na umri wa rais wa nchi unasababisha umasikini kwa watoto wetu mitaani? Umri wa rais unasababisha watoto wa mitaani ambao kwa matendo yetu tunaunda janga?

Kwamba riba ya madeni barani Afrika inasababishwa na umri wa watawala wake? Kupangwa kwa kukua au kushuka thamani ya fedha ya taifa kutokana na umri wa rais wa nchi?

Ni siku nyingi sana na wala si jambo geni kuona kwamba wanahistoria na wataalamu mbalimbali wakisema Bara la Afrika ni masikini, vita na habari hasi kwa wingi. Lakini hakuna mtu anayejiuliza inakuwaje bara moja likakabiliwa na matatizo yote hayo.

Ndiyo maana waliokata tamaa ya kuona maendeleo ya bara hili wamerukia hoja nyepesi kuwa umri wa watawala wa Afrika ni mkubwa hivyo unazorotesha maendeleo yetu.

Jared Diamond wa jarida la National Geographic katika andiko lake la “The Shape of Africa”, anauliza swali hilo, kwamba inakuwaje yote haya yawe tatizo kwa Afrika ikiwa nchi nyingine zinakuwa na watawala wenye umri mkubwa?

Anaeleza, “vyovyote unavyoweza kusema, lakini Afrika ni sehemu ambayo ilianza Homo Sapiens hadi wataalamu wakaita hilo ni ‘mfumo wa tabia za kisasa’. Watu wote wanao ubongo huo ambao ulisambaa hadi Ulaya na Asia. Uholanzi na Asia kuna Hominis na ilijulikana kuwa chanzo cha uwepo wa mwanadamu. Afrika ilifurahia miongo mitatu ya historia ya mwanadamu, lakini nyakati hizi si bara lile lenye histori tamu kulinganisha na miaka 10,000 iliyopita.”

Sote tunajua kuwa Afrika ni kiini cha taaluma mbalimbali zilizojitokeza duniani miaka ya baadaye kwa nchi nyingine, lakini nini kinatufikisha hadi kuaminishana kwamba umri wa watawala wetu ni kikwazo au chanzo cha maendeleo hafifu ya bara hili?

Maradhi yaliyotamalaki ya malaria, Ukimwi, manjano na ugonjwa wa kulala, yamekuwa sehemu ya maisha ya watu wa Bara la Afrika. Ni lazima tujitazame kwenye mambo ya msingi kuliko kukurupukia umri wa viongozi wetu.

Ili kupata ahueni ya maendeleo ni lazima tuwekeze kwenye sekta ya afya ya watu wetu ili waweze kuleta mabadiliko. Pia, suala la teknolojia si la kupuuza, hivyo kukubali kwamba tunatakiwa kuingia kwenye utandawazi kwa umakini ni lazima tukubali kuwa nyakati nyingine tutaumizwa kwayo. Hatuna sababu ya kusingizia umri wa watawala wetu kuwa ni kikwazo cha maendeleo Afrika.

Hatuna sababu ya kulalamikia umasikini wetu, ni lazima tuchukue hatua. Lazima tuseme kuwa hatukuumbwa ili tuwe masikini. Lazima tuketi chini na kuona kuwa katikati ya umasikini wetu kuna fursa ambazo zinawezesha kuikwamua jamii. Ni lazima tuseme umri wao ni tarakimu tu, sawa na hisabati ya kujumlisha, kutoa, kugawanya na kadhalika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles