NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), , amesema atahakikisha shirika hilo linapitia upya mikataba ya wabia wa madini ili kuondokana na mikataba mibovu isiyokuwa na tija.
Balozi Muganda aliyasema hayo jana alipokuwa akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo Dar es Salaam na kuongeza kuwa Stamico inakabiliwa na changamoto kubwa ya miradi kushindwa kusimamiwa vyema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, alimuagiza Balozi Muganda kuhakikisha anafuatilia miradi yote inayomilikiwa na shirika hilo.
Profesa Ntalikwa alisema ili shirika hilo liweze kufanikisha mipango ya Serikali ni lazima miradi inayomilikiwa na shirika ikasimamiwa ipasavyo.
Alisema sera ya madini ya mwaka 2009 inasisitiza ongezeko la ushiriki wa Serikali na wananchi katika shughuli za madini ili kuongeza manufaa yatokanayo na madini.
“Kutokana na mtazamo huo wa Serikali Stamico imepewa jukumu la kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta ya madini kwa niaba ya Serikali, hivyo bodi bado ina wajibu mkubwa wa kulisimamia hili kwa manufaa ya taifa,” alisema.