22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

Maliasili yapewa ndege nane  

MaghembeNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameiomba jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupiga vita ujangili kwa vitendo ili kuimarisha uhifadhi nchini.

Alisema hayo jana wakati wa hafla ya makabidhiano ya ndege maalumu nane zilizotolewa na Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) katika eneo la  Matambwe Selous.

Ndege hizo ndogo aina ya Drones ambazo hazitumii rubani – huongozwa na mitambo maalumu, zitatumika katika pori la akiba la Selous kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa wanyamapori kwa kukusanya taarifa za kiintelijensia zitakazosaidia kukamatwa majangili.

Ndege zote zina thamani ya dola za Marekani 80,000  ambazo ni sawa na zaidi ya Sh milioni  172.

“Msaada huu umekuja wakati mwafaka, pori la akiba la Selous linahitaji teknolojia za kisasa kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili ndani na kuzunguka hifadhi hii,” alisema Profesa. Maghembe.

Alisema changamoto kubwa inayoikabidili hifadhi ya Selous ni ujangili ambao kwa kiasi kikubwa umesababisha wanyama kama tembo kupungua kwa kasi kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Profesa Maghembe alisema takwimu zinaonyesha mwaka 1986, idadi ya tembo katika pori hilo ilikuwa 50,000, ambayo iliongezeka mwaka 2003 na kufikia 70,000, baada ya Serikali ya Ujerumani kusaidia kuanzishwa mpango wa kuendeleza Selous na Serikali ya Tanzania kukubali asilimia 50 ya makusanyo yanayotokana na utalii yabaki kuendeleza uhifadhi katika pori hilo.

Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Mabula Misungwi, alisema baadhi ya changamoto kuu zinazoikabili hifadhi hiyo ni pamoja na ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa ikiwemo magari ya doria na nyumba za watumishi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WWF, Dk. Marco Lambertini, alisema ili kuimarisha uhifadhi nchini, ni lazima wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo washirikishwe ili wasaidie kuyalinda kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,283FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles