Na Renata Kipaka, Kagera
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, ametangaza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Geita na Kagera utaanza rasmi Agosti 5 hadi 11, 2024. Jaji Mwambegele alitoa taarifa hiyo wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika Julai 24, 2024, mkoani Kagera.
Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk, ukiwa ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha mikoa ya Kagera na Geita, na uboreshaji utaanza tarehe 5 hadi 11 Agosti, 2024,” alisema Jaji Mwambegele. Aliongeza kuwa mzunguko huu wa pili unafuatia mzunguko wa kwanza uliyojumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi, na Tabora, ambapo uboreshaji ulianza tarehe 20 Julai, 2024 na unatarajiwa kukamilika leo, tarehe 26 Julai, 2024.
Jaji Mbarouk, akizungumza mkoani Kagera, alisisitiza kuwa kadi za wapiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 ni halali na zitaendelea kutumika katika chaguzi zijazo. Aliwataka wadau wa uchaguzi kuwaelimisha wapiga kura wenye kadi hizo wasiende kuboresha taarifa zao kwani zoezi hilo haliwahusu.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo. Hivyo, zoezi hili la uboreshaji wa Daftari haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo,” alisisitiza Jaji Mbarouk.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhan, akizungumzia teknolojia ya uandikishaji wa wapiga kura wakati wa kuwasilisha mada, alibainisha kuwa wapiga kura wanaotaka kuboresha taarifa zao wanaweza kuanza mchakato huo kwa kutumia simu janja, kiswaswa, au kompyuta kupitia mfumo unaojulikana kama Online Voters Registration System (OVRS) au kwa kubofya *152*00#, kisha namba 9 na kufuata maelekezo.
“Mtumiaji wa huduma hii atatakiwa kufika kituoni anachokusudia kujiandikisha ili kukamilisha hatua za kupigwa picha, kuweka saini, na kupatiwa kadi yake ya mpiga kura,” alieleza Bw. Kailima.