Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema kumekuwa na ongezeko la wawekezaji wa ndani Watanzania ambao wamesajili miradi yao TIC mwaka jana kwa asilimia 38, huku Watanzania walioshirikiana na wageni wabia ikiwa ni asilimia 20. Hii inamaanisha kuwa asilimia 58 ya miradi iliyosajiliwa katika kituo hicho kwa mwaka uliopita ni ya ndani.
TIC imemtaja Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa Shujaa Namba Moja wa Uwekezaji, akijipambanua kwa kufanya uwekezaji kuwa moja ya nyenzo muhimu ya kuwaletea maendeleo Tanzania, ikiwemo kuongeza ajira nchini.
Hayo yamesemwa leo Julai 25 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, wakati wa Mkutano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wawekezaji wa Ndani uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Teri alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuwaeleza wawekezaji kuhusu nafuu zilizowekwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia ili kurahisisha na kusaidia kuanzisha uwekezaji na biashara zao kwa urahisi.
“Juhudi za Rais Samia zimepelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la uwekezaji wa ndani wa Tanzania, ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 kituo cha uwekezaji kilisajili miradi 707, ambayo ni ongezeko la asilimia 91 ukilinganisha na miradi 360 iliyosajiliwa mwaka wa fedha 2022/23,” alisema Teri.
Aliongeza kuwa hilo ndio lengo la Rais Dk. Samia alipobadilisha sheria ya uwekezaji mwaka 2022, na tangu kuanzishwa kwake kituo hiki mwaka 1997, hii ni mara ya kwanza Watanzania wenyewe wananufaika na vivutio vya uwekezaji vilivyopo katika kituo hicho.
Naye Meneja wa Utafiti na Mipango wa TIC, Anna Lyimo, alisema takwimu za TIC zinaonyesha kwamba sekta ya usafirishaji ina asilimia kubwa ya wawekezaji wa ndani. Ameeleza kuwa kumekuwa na maboresho ya serikali ambayo yamelenga kusaidia wawekezaji wa ndani kujisajili TIC na kunufaika na vivutio vya kodi vinavyotolewa na serikali.
TIC imemtaja Shujaa wa Pili Mtanzania, ambaye ni mwekezaji wa ndani aitwaye Amir Hamza, aliyeanza kufanya uwekezaji tangu mwaka 1994, na katika kituo cha uwekezaji wanamthamini kama shujaa.
Kwa upande wake, Mwekezaji wa Ndani, Amir Hamza, alisema Rais Dk. Samia amefanya kazi nzuri kuhamasisha uwekezaji, ambapo kupitia mkutano huo wamefanikiwa kuelewa sheria na kanuni mpya zilizobadilishwa tangu mwaka 2022 na ambazo zinalinda na kuhamasisha wawekezaji wa ndani kuweza kuwekeza katika nchi yetu wenyewe.