32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wakaribishwa kutembelea banda la TFS maonyesho ya Sabasaba

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki umetoa rai kwa wananchi kujitokeza kwenye banda lao ili waweze kujifunza na kufaidika na ofa zinazotolewa kwa watakaohitaji kutembelea hifadhi za misitu zilizopo nchini.

Akizungumza Julai 1, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Kuhamasisha Utalii wa TFS, Anna Lauwo, alipotembelea banda lao lililopo kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula, alisema hifadhi za misitu nchini zimekuwa na vivutio mbalimbali, ikiwemo bwawa lenye muonekano wa ramani ya Afrika.

“Hifadhi zetu zimekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii na ndiyo maana hapa tunatoa kifurushi ambacho tunaweza kumpatia mtu yeyote anayetaka kutembelea hifadhi zetu. Akija hapa tutamsaidia na kwa bei rahisi sana anaweza kwenda kujionea na kujifunza kwa vitendo,” amesema Lauwo.

Kwa upande wake, Afisa Ufugaji Nyuki TFS, Said Abubakar, alisema kufuatia umuhimu wa ufugaji nyuki nchini, wameanza kutoa elimu kwa watoto ili kuleta hamasa ya ufugaji nyuki lakini pia kuzidi kuifanya nchi kuendelea kuzalisha asali bora duniani.

“Tunapokea watoto wa miaka miwili mitatu ili tuwatengezee hamasa ya ufugaji nyuki kwani wakiwapenda nyuki watafuata masomo yanayotokana na ufugaji nyuki, watatunza mazingira na kupanda maua ya kutosha lakini pia wataelewa umuhimu wa mdudu nyuki,” amesema.

Pia, Abubakar ametoa wito kwa shule mbalimbali nchini kuanzisha klabu za ufugaji nyuki kama zilivyo klabu nyingine za masomo ili kuendelea kutoa elimu ya ufugaji huo.

Amesema TFS kupitia ofisi zao za kanda wamekuwa wakipokea maombi mbalimbali ya kutoa elimu kwa shule lakini pia wanaendelea kutoa elimu kwa mtu mmoja mmoja na vikundi pindi wanapotembelea kwenye ofisi zao.

“Nipende kutoa rai kwa shule za serikali na shule binafsi kutengeneza klabu za ufugaji nyuki kwani muda muafaka sasa sisi tupo na tutakuwa tunawatembelea huko na kutoa elimu,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa hadi sasa wana shule moja ambayo inaendesha klabu hiyo.

Akizungumzia ujio wa mkutano mkubwa wa kimataifa wa wadau wa ufugaji nyuki unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha mwaka 2027, amesema wamejiandaa vizuri na hivyo wageni wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo watajionea namna walivyojipanga katika ufugaji na mnyororo mzima wa thamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles