28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi wa Mvomero waunga mkono juhudi za Rais Samia kutangaza Utalii

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Watumishi wa kada mbalimbali wa Wilaya ya Mvomero, wakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Saidi Nguya, wameunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii nchini kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Julai 6, 2024, Saidi Nguya alisema, “Dk. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa, ndiyo maana amekuja na program ya Royal Tour kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini.”

Nguya aliongeza kuwa Rais Samia amefanya kazi kubwa kwa nafasi yake, hivyo watumishi wa Wilaya ya Mvomero wanawajibu wa kuhamasishana ili kuonyesha mchango wao katika kutangaza na kuhamasisha utalii. “Sisi kwa nafasi yetu hapa kwenye ngazi ya Wilaya, Kata, Tarafa, na Vijiji tunawajibu wa kuhamasishana sisi kwa sisi tuoneshe mchango wetu,” alisema Katibu Tawala.

Katibu Tawala huyo alibainisha kuwa moja ya majukumu yao kama wasaidizi wa Rais ni kutafsiri maono yake kulingana na mazingira waliyopo. Aliongeza kuwa ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuwapa nafasi wahudumu, waandishi waendesha ofisi, na watunza kumbukumbu kutoka taasisi mbalimbali za Wilaya hiyo kupumzika na kufurahia kutokana na kwamba kundi hilo mara nyingi halitazamwi vizuri.

“Ubora wa ofisi unaanzia kwa kundi hili kwa sababu linapokea wateja wengi. Hivyo, kundi hili linatakiwa kupewa kipaumbele ili kupunguza ama kuondoa kabisa malalamiko ya wateja kuhusu ofisi au taasisi husika,” alisema Saidi.

Afisa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, David Kadomo, aliwapongeza watumishi hao kwa ziara yao, akisema wanahamasisha utalii wa ndani na kutoa wito kwa Wilaya zingine kuiga mfano wa Mvomero. Kadomo aliongeza kuwa sekta ya utalii inachangia zaidi ya asilimia 17 kwenye pato la taifa, hivyo kuna umuhimu wa kutunza hifadhi.

Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi, hali ambayo imechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii kufikia 100,033 katika hifadhi ya Mikumi kwa mwaka huu.

Watumishi wa Wilaya ya Mvomero, akiwemo Issaya Ramson, ambaye ni Mtunza Kumbukumbu, alisifu juhudi za Rais Samia za kuhamasisha utalii nchini na kutoa wito kwa Wilaya zingine kutembelea hifadhi hiyo. Ramson alibainisha kuwa hifadhi hiyo ina wanyama mbalimbali kama vile tembo, twiga, swala, pundamilia, nyoka, na ndege mbalimbali.

Raheli Mgoni, Mwandishi Mwendesha Ofisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, alisema kuwa ziara hiyo imewapa fursa ya kubadilishana uzoefu na watumishi wengine na kujifunza masuala ya kitalii.

“Jambo la watumishi, hususani wa kada za waandishi waendesha ofisi, wahudumu, na watunza kumbukumbu kutembelea hifadhi ya Mikumi, halijawahi kufanyika. Hivyo, siku ya leo ni ya kipekee,” alisema Mgoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles