28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

TVLA yazindua Teknolojia za kisasa kukabiliana na magonjwa ya wanyama

Na Grace Mwakalinga?Mtanzania Digital

Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeanzisha teknolojia za kisasa za kitaalam kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya wanyama. Miongoni mwa teknolojia hizi ni matumizi ya vina saba, ambapo sampuli za wanyama huchukuliwa na kupimwa ili kugundua aina ya magonjwa yanayowasumbua.

Teknolojia hii ni moja ya huduma zinazotolewa na TVLA, zikilenga kufanya utambuzi sahihi wa magonjwa yote ya wanyama na kutoa tiba stahiki. Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dk. Stella Bitanyi, alieleza hayo kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

“Lengo letu ni kubuni na kutumia teknolojia mbalimbali kwa ajili ya kuhudumia wanyama wetu. Uvumbuzi wetu unalenga kutatua matatizo ya kiafya yanayoikumba mifugo. Ni muhimu wadau wa ufugaji kutembelea banda letu na kujifunza kuhusu huduma zetu,” alisema Dk. Stella.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dk. Stella Bitanyi (kushoto) akitoa elimu kwa mdau wa Mifugo kuhusiana uchunguzi wa magonjwa ya minyoo inayoathiri afya za Mifugo ili kuweza kuitambua na kushauri dawa zinaweza kutibu minyoo hiyo kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Julai 05, 2024.

Akiendelea kufafanua, Dk. Stella alisema kuwa wanatoa elimu kuhusu umuhimu wa uchanjaji wa mifugo, utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, utafiti wa magonjwa, na ushauri kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo.

Aidha, TVLA inatoa elimu ya udhibiti wa wadudu aina ya mbung’o ambao hueneza ugonjwa wa Nagana, pamoja na magonjwa yaenezwayo na kupe kama ndigana kali na ndigana baridi. Wanahakikisha ubora wa viuatilifu vya kuogesha wanyama ili kudhibiti kupe.

Wadau wa mifugo waliotembelea banda la TVLA wamefurahishwa na huduma zinazotolewa, hususan elimu ya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo kabla ya kuwatibu na elimu ya uchanjaji wa mifugo. Walisema walikuwa wakichanja mifugo yao bila kuipima, jambo lililosababisha vifo kwa mifugo yao.

Mtaalam wa Mifugo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Henri Mlundachuma (kushoto) akitoa elimu kwa mdau wa Mifugo alietembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusiana na uoteshaji wa vimelea vya bakteria (Media) kwa kutumia petri dishi kwa ajili ya kutambua dawa yenye ufanisi mzuri wa kutibu ugonjwa uliogundulika kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar Es Salaam (Sabasaba) Julai 05, 2024.

Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanakutanisha wafugaji, wakulima, wafanyabiashara, na wajasiriamali kutoka nchi mbalimbali duniani. TVLA imeshiriki kwa kuonesha teknolojia mbalimbali za kitaalamu na za kiubunifu kwa ajili ya kuboresha afya ya mifugo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles