27.6 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Msako umekomesha watoto kuzagaa mitaani wakati wa masomo

Na Patricia Kimelemeta, Mtanzania Digital

“Nilikamatwa kwa sababu sikumpeleka mwanangu shule kuanza darasa la kwanza,” anasema Mwajuma Selemani mkazi wa Mbagala kibongemaji iliyopo Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza hivi karibuni, Mwajuma anasema kuwa, mwezi wa kwanza kunakua na msako wa watoto wasiokwenda shule na mwanae wa kike mwenye umri wa miaka minane alikua miongoni mwa watoto wasioandikishwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo umaskini na hali ngumu ya maisha.

“Ilifika wakati hata fedha ya kununua unga robo sina, mtoto anatakiwa aende shule, umnunulie sare za shule, viatu, madaftari na vifaa nyingine, hali ngumu ya maisha ilinifanya nisimpeleke mwanangu kusoma, msako ulipoanza wa nyumba kwa nyumba nilikua sina taarifa, nikajishtukia nipo kwa mtendaji chini ya ulinzi wa polisi na maofisa Ustawi wa jamii,” anasema Mwajuma.

Anaongeza kuwa, kutokana na hali huyo alilazimika kupambana huku akiomba msaada kwa ndugu na jamaa ili kuhakikisha mtoto anakwenda shule jambo ambalo alifanikiwa.

Ameongeza kuwa, kitendo cha Serikali kuweka msako wa nyumba kwa nyumba kimesaidia kupungua kwa watoto kuzagaa mitaani wakati wa siku za masomo.

“Sasa hivi hakuna watoto wanaozagaa mitaani siku za masomo hasa hawa wadogo wanaosoma chekechea na madarasa ya awali kwa sababu watendaji wanapita nyumba kwa nyumba na wakiwakuta watoto, mzazi au mlezi unakamatwa,” amesema.

Ameongeza kuwa, utaratibu huu ni mzuri kwa sababu unawahamasisha wazazi kuona umuhimu wa kuwapeleka watoto shule kwa hiari waweze kupata elimu. Katibu wa Umoja wa Vituo vya kulea watoto mchana (DCC), Josephine Mushumbushi anasema kuwa, mwamko wa wazazi au walezi kupeleka watoto wenye umri wa kuanzia miaka miwili hadi sita kwenye vituo hivyo umeongezeka.

Amesema kuwa, hali hiyo imetokana na Serikali kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuona umuhimu wa kuwapeleka watoto kwenye vituo hivyo na wale waliofikia umri wa kuanza darasa la awali na la kwanza wapelekwe shule.

“DCC imekua ikipokea watoto kuanzia umri wa miaka miwili ili waweze kupata fursa ya kujifunza na kwamba wanapofika umri wa miaka mitano wanaanza darasa la awali na wakifika sita au saba wanaanza darasa la kwanza.

“Hali hiyo inasaidia kumjenga mtoto kisaikolojia, kupenda kujifunza na kupenda kusoma pale anapoanza shule ya msingi, hivyo basi tunapaswa kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanajitokeza kupeleka watoto kwenye vituo hivyo,” amesema Mushumbushi.

Ofisa Elimu, Awali na Msingi wa Manispaa ya Ubungo, Mwalimu Denis Nyoni amesema kuwa, mwaka huu kumekua na ongezeko kubwa la watoto walioandikishwa kuanza darasa la awali na la kwanza.

“Mwaka 2023 Manispaa ya Ubungo imeweza kuandikisha watoto 4919 ambao walijiunga na darasa la awali lakini mwaka huu tumeweza kuandikisha zaidi ya watoto 7797.

“Kwa upande wa darasa la kwanza, Mwaka 2023, Halmashauri tuliandikisha watoto 19616 na Mwaka huu zaidi ya watoto 18,650 waliandikishwa,”amesema Mwalimu Nyoni.

Ameongeza kuwa, uandikishwaji huo umeenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya madarasa ili kuwawezesha watoto kusoma katika mazingira tulivu na salama kulingana na umri wao kuwa mdogo.

Amesema kuwa, maboresho hayo yametokana na fedha kutoka serikali kuu, fedha za mapato ya ndani ya halmashauri na wadau mbalimbali. Amesema kuwa lakini pia wamekua wakishirikiana na wadau mbalimbali ili kuwezesha watoto kupata vifaa vya kujifunzia ikiwamo kuwawekea kona nne za kujifunza (KKK) katika madarasa yao pamoja na vifaa vingine vya kusoma.

“Lakini pia tumeweza kushirikiana na wazazi kutengeneza zana za mikono ambazo watoto wanazitumia wakati wa kujifunza. Mwalimu Nyoni amesema kuwa, wadau hao wameweza kutoa mafunzo kwa walimu wa madarasa ya awali na la kwanza ili waweze kujua namna ya kulea watoto hao pamoja na kuwatambua ikiwa watabainika kuugua ghafla wakiwa shuleni, waweze kuwasiliana na wazazi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya haraka.

“Wazazi wamekuwa mstari wa mbele kuchangia chakula shuleni hapo ambapo watoto wanapikiwa kwa kufuata mwongozo uliotolewa na Taasisi ya chakula na Lishe nchini. Ukiangalia tulipotoka na tulipo hali ni tofauti, sasa hivi kuna mwamko mkubwa wa elimu kwa wazazi ndomana wamekuwa wepesi kushirikiana na serikali kuangalia namna bora ya malezi ya watoto wawapo shuleni,” amesema.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha amewataka wazazi na walezi kuwa makini na watoto pindi wanapokwenda au kurudi shuleni.

“Ulinzi wa mtoto unaanza na mzazi au mlezi, unafuata na jamii husika pale ambapo mtoto anapoishi, anapokwenda shule au kwenye kituo cha kulea watoto mchana anapaswa kulindwa ili aweze kupata fursa ya kujifunza na kurudi nyumbani akiwa katika hali ya usalama,” amesema Nyamara.

Naye Mtaalamu wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka Tasisi Isiyo ya kiserikali ya children In Crossfire (CIC), Davis Gisuka amesema kuwa, licha ya kuwepo kwa ongezeko hilo, serikali inapaswa kuboresha miundombinu ya shule ili iwe rafiki kwa watoto na hata wale wenye ulemavu.

“Licha ya serikali kuboresha miundombinu lakini kumekua na changamoto ya uhaba wa walimu wa malezi ambayo ndiyo wenye jukumu la kulea watoto,” amesema Gisuka.

Amesema kuwa, lakini pia watoto wenye ulemavu wamekuwa wakisahaulika kupatiwa mahitaji yao ikiwamo vifaa ya kujifunzia kwa wale wenye tatizo la usikivu na wale wasioona wanaotumia nukta nundu.

Amesema kuwa, ikiwa serikali itahakikisha vifaa hivyo vinapatikana kwa wakati, wataweza kutoa fursa sawa ya kujifunza kwa watoto wenye changamoto za ulemavu na wale wasio na changamoto hizo. Ameongeza kuwa, serikali pia inapaswa kuboresha miundombinu ya ya vyoo ili kwa watoto hao ili waweze kutumia vya kwao peke yao bila ya kuchangia na wanafunzi wa madarasa ya juu kwa ajili ya kuwaepusha nna magonjwa hatarishi.

“Watoto wadogo wanaweza kujisaidia popote, ikiwa watachangia vyoo na wakubwa, wanaweza kupata magonjwa na kuhatarisha afya zao, hivyo basi serikali wakati wanaboresha miundombinu ya madarasa wanapaswa kwenda sambamba na ujengaji wa vyoo vya watoto wadogo,”amesema Gisuka.

Kwa upande wake, Afisa Lishe kutoka Mkoa wa Dar es salaam, Mwamvua Zuberi anasema kuwa, Serikali imetoa mwongozo wa lishe kwa watoto wadogo ili waweze kula vyakula vyenye virutubisho, jambo ambalo litawasaidia kukuza ubungo na kuwa na uelewa mzuri.

“Ikiwa watoto watapatiwa vyakula vyenye virutubisho wakiwa shuleni, watapenda kusoma na ufaulu utaongezeka, ndomana kila shule imepewa mwongozo wa lishe ambao wanatakiwa kufuata,” amesema.

Anasema kuwa baadhi ya wananchi wanasema kuwa, serikali imekuwa ikishirikiana na watendaji wa kata na mtaa kupita mitaani kwa ajili ya kukagua watoto wasiokwenda shule, hali huyo ni tofauti na miaka iliyopita na ndomana kumekua na ongezeko kubwa.

“Siku hizi ikibainika kuna mtoto hasomi nyumbani kwako jela inakuita, ikifika mwezi wa kwanza, utaona watendaji wa kata na mtaa wanapita nyumba hadi nyumba kwa ajili ya kuangalia watoto wasiokwenda shule, wazazi au walezi wao wanaitwa kwa mtendaji na kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema Omary Khamis mkazi wa Tandale iliyopo Manispaa ya Kinondoni.

Hata hivyo, Serikali ilizindua Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) mwaka 2021 ambayo inamalizika mwaka 2026 na afua tano za afya, elimu, lishe, malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles