Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
DUNIA ni kama ‘imepigwa na kitu kizito’ kufuatia janga la virusi vya Corona lilodumu tangu mwishoni mwa mwaka juzi.
Si Kusini wala Kaskazini mwa dunia, ambako janga hili halijaacha athari, kila nchi imetikiswa kwa namna yake.
Hata hivyo, kutokana na uharaka na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, chanjo ya janga hilo tayari imepatikana na inaendelea kutumika kwenye mataifa mbalimbali, Tanzania ikiwa ni miongoni.
Tanzania imekuwa sehemu ya nchi chache zilizopata chanjo hiyo kupitia mpango wa Covax, lengo likiwa ni kuziwezesha kumudu gharama za chanjo hizo.
Takribani dozi 1,005,400 aina ya Johnson and Johnson zimepolewa nchini na zoezi la uchanjaji linaendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini tangu mikoa mbalimbali ilipoanza kuzindua utoaji wa huduma hiyo Agosti 4, mwaka huu.
Takwimu za mwisho za utoaji wa chanjo zilizotolewa Agosti 15 na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinaonesha kuwa jumla ya walengwa 207,391 wamechanjwa kwa hiari kwenye vituo 550 vilivyotengwa nchi nzima.
Hata hivyo, kwa kipindi chote cha elimu ya kujikinga na Corona, bado kuna kundi lililosahaulika, licha ya kuwa kwenye mazingira hatarishi.
Hilo si kundi jingine bali ni lile la watoto wa mitaani, ambao mara zote huonekana kwenye makutano ya barabara, hasa kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.
Iko wazi kuwa bado hakuna sauti inayojitokeza kulisaidia kundi hili katika kuhakikisha linakuwa salama kwa kipindi hiki dunia ikiendelea na mapambabo dhidi ya Corona.
Kwani kama tunavyofahamu, kundi hili ndilo lililoko kwenye hatari kubwa kutokana na kukutana na watu tofauti.
Ukweli ni kwamba vijana hawa wana hatari kubwa ya kubeba maambukizi kutokana aina ya utafutaji wao wa rikizi.
Ndiyo, mazingira ya kuomba fedha kwa wapitajinjia na abiria, yanawaweka kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo.
Aidha, kwa kugusa magari pindi wanapokuwa wanasaka mkate wao wa kila siku, ni wazi wanahitaji kulindwa si tu kwa kupewa elimu, bali pia vifaa zikiwamo barakoa.
Ieleweke kuwa jamii haitakuwa imefanikiwa kujilinda kwa asilimia 100 na Corona ikiwa watoto wa mitaani wataendelea kuwa kwenye mnyororo wa maambukizi.
Mwisho, mamlaka, hususan za majiji, likiwamo hili la Dar es Salaam, ziliangalie kundi hili kwani bado lina uwezo mdogo wa kujisimamia kimaamuzi kutokana na umri mdogo walionao.
Katika hilo, Ramadhan (9), ni miongoni mwa watoto wanaoishi kwa kuombaomba kwenye Mataa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Sisi tunaona tu watu wanazungumzia lakini hatujafuatwa,” anasema Ramadhan anayekiri pia kuona watu wakiwa wamevaa barakoa.
“Unajua kaka, mimi naona tu watu wengine wamevaa barakoa, wengine za vitambaa, wengine za saresare (akimaanisha za dukani) wanasema ni kwa ajili ya Corona.”
Wakati huo huo, anasema wanatamani kupata barakoa lakini kikwazo kikubwa kwao ni kipato cha kumudu kuzinunua.
Kwa upande wake, Omari (15) anaungana na mwenzake huyo na kusema wako tayari kutoa ushirikiano endapo itakuwapo programu ya kuwapa elimu ya Corona.
“Tunatamani tungepata msaada wa hiyo elimu tunayoisikia huko kwa watu kwani sisi ni kama tumeachwa,” anasema na kuongeza: “Serikali itukumbuke na sisi watoto wa mitaani, hatuishi huku kwa kupenda,” anasema Omari.
Kama ambavyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, anavyohimiza mapambano dhidi ya Corona, basi hana budi kuliangalia kundi hili kwa ukaribu ili kuona litakavyowezeshwa kuepuka maambukizi.
Mwisho, katika kundi hili lipo wapo vijana wenye umri stahiki kwa chanjo ya Corona inayoendelea kutolewa hapa nchini.
Kwanini wale waliofikia umri huo wasiandaliwe utaratibu maalumu wa kupata chanjo (kwa watakaopenda)?