27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hili lilisahaulika au halikupangwa Siku ya Wananchi?

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KAMA wasemavyo, Wananchi hawana jambo dogo. Ndicho walichokithibitisha jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Ilikuwa ni zaidi ya uwanja ‘kutapika’.

Wingi ule wa mashabiki na wanachama ulikuwa na maana mbili kubwa. Mosi, Yanga inaweza kukosa kila kitu lakini si mtaji wa watu. Kwamba jukumu linabaki kwa viongozi, kuhakikisha wanatengeneza daraja litakalounganisha wingi wa mashabiki na uchumi wa klabu.

Pili, ulikuwa ni ujumbe kwa benchi la ufundi na wachezaji wa Yanga. Kwa timu ambayo haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu minne, ungetegemea idadi ndogo ya mashabiki Siku ya Wananchi.

Kinyume chake, wingi ule pale Benjamini Mkapa unamaanisha mashabiki wa Yanga hawajakata tamaa. Kwamba wanaamini msimu huu (2021-22) ni wao, iwe isiwe!

Tuachane na hayo na mengi yaliyojitokeza jana, ikiwamo lejendari wa Rhumba, Koffi Olomide, kupanda jukwaani na kuingia kwenye historia ya kilele cha Siku ya Wananchi.

Kama nilivyotanguliza, haitakuwa rahisi kutaja yote lakini nikiri kuvutiwa zaidi na utaratibu uliojitokeza wakati wa mapumziko ya mechi kati ya Yanga na Zanaco, ambayo ilimalizika kwa wenyeji kufungwa mabao 2-1.

Naizungumzia hatua ya klabu ya Yanga kuwapa tuzo wachezaji wake waliofanya vizuri msimu uliopita. Tuzo ya Mchezaji Bora ilikwenda kwa Mukoko Tonombe. Ile ya Mfungaji Bora ilitua kwa Yacouba Sogne. Kibwana Shomari aliibeba tuzo ya Chipukizi Bora klabuni hapo.

Ukweli usio na shaka ni kwamba lilikuwa jambo zuri kutambua mchango wa kila aliyepambana kwa ajili ya timu. Hii inakwenda kuimarisha saikolojia yao, pia ikiongeza kasi ya upambanaji kwa wale waliokosa.

Hata hivyo, kile kilichonisukuma kuja na andiko hili ni kutoona mchango wa wachezaji wa timu ya soka ya wanawake ya Yanga (Yanga Queens) ukitambuliwa kwenye utoaji wa tuzo hizo.

Ni kwamba msimu uliopita ulikuwa mbaya zaidi kwa Yanga Princess na kuifanya klabu isione mchezaji anayepaswa kupewa tuzo Siku ya Mwananchi? Siamini.

Timu iliyoshika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa, Simba Queens, inakosaje mchezaji bora wa kikosi? Ilimalizaje msimu ikiwa ya pili huku ikiwa haina mchezaji mwenye wastani mzuri wa mabao?

Sitaki kuamini hilo lakini wengine walioshuhudia kile kilichofanyika wangeweza kutafsiri kitendo hicho ni upande mwingine wa klabu ya Yanga kupuuza soka la wanawake.

Kama si hivyo, huenda inaweza kushusha morali ya wachezaji wa Yanga Queens, sambamba na benchi lao la ufundi. Ilishika nafasi ya pili, kama ilivyo timu ya wanaume. Kwanini wenzao waonekane bora zaidi, tena siku muhimu kama ile?

Naomba kuwasilisha…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles