32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

UONGOZI CHADEMA WALALA JELA

SAFU ya juu ya uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wenzake watano wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka nane yakiwemo mawili ya uchochezi wa uasi yanayomkabili Mbowe.

Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo viongozi hao wote walikosa dhamana na kupelekwa Gereza la Segerea hadi kesho (Machi 29), ambapo mahakama itatoa uamuzi wa dhamana yao au laa.

Washtakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Dk. Zainabu Mango na Faraja Nchimbi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon.

Miongoni mwa mashtaka nane, Mbowe yumo katika mashtaka saba ambapo matano yakiwemo ya uchochezi wa uasi yanamkabili peke yake.

Wakili Nchimbi aliwataja viongozi hao wa Chadema ambao walifikishwa mahakamani hapo saa tisa mchana chini ya ulinzi mkali wa polisi wakitokea Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam  ambao ni Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji na manaibu wake wa Bara na Zanzibar, John Mnyika na Salum Mwalimu.

Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, ambapo wote mapema asubuhi walikwenda kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambako walifutiwa dhamana na kupelekwa mahabusu.

Vigogo hao wa Chadema baada ya kufikishwa mahakamani hapo kwa kutumia gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser huku kukiwa na magari mengine mawili ya polisi yenye askari walipelekwa mahabusu ya mahakama hiyo.

Washtakiwa wote walisomewa mashtaka ya kufanya mkusanyiko au maandamano yasiyo halali, kuendelea na mkusanyiko usio halali wenye vurugu baada ya kutolewa tamko la wao kutawanyika.

Mbowe peke yake alisomewa mashtaka kuhamasisha chuki miongoni mwa wanajamii isivyo halali, uchochezi na kusababisha chuki miongoni mwa wanajamii, uchochezi wa uasi, ushawishi utendekaji wa kosa huku Msigwa akisomewa shtaka la kushawishi raia kutenda kosa.

Wakili Nchimbi alidai mahakamani hapo kwamba washitakiwa wote Februari 16, mwaka huu, wakiwa katika Barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja kinyume cha sheria, waliendelea na mkusanyiko katika namna iliyowafanya watu waliokuwa kwenye eneo hilo waogope na kwenda kwenye uvunjifu wa amani.

Inadaiwa washtakiwa wote katika tarehe hiyo wakiwa kwenye barabara hiyo kwa pamoja katika ujumla wao wakiwa wamekusanyika na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani wakiwa katika maandamano au mkusanyiko wenye vurugu na kutozingatia amri ya kusitisha maandamano waligoma kutawanyika na kuendelea na mkusanyiko huo wa vurugu uliosababisha kifo cha Akwilina Akwilin na majeraha kwa askari wawili kutokana na mkusanyiko wa vurugu.

Mshtakiwa  Mbowe anadaiwa siku hiyo katika viwanja vya Buibui, vilivyoko wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, akiwa anahutubia wakazi wa Kinondoni alitoa matamshi ambayo kwa hali ya kawaida yanaleta hisia za chuki miongoni mwa wanajamii na wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mbowe anadaiwa kusema: ‘Ninapozungumza hapa kiongozi wetu wa Kata ya Kinondoni Hananasif yupo mochwari… amekamatwa na makada wa CCM kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama… Wamemnyonga wamemuua halafu sisi tunaona ni jambo la kawaida… Tunacheka na polisi na CCM’.

Katika mashtaka ya uchochezi wa uasi, Mbowe anadaiwa siku hiyo kwenye viwanja hivyo alitoa maneno kwa nia ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa wananchi dhidi ya mamlaka halali ya Serikali iliyoko madarakani.

Anadaiwa kusema: ‘Tumejipa kibali cha kutangulia mbele ya haki… Haiwezekani wanaume wazima na akili zetu na wake zetu na watoto wetu tukafanywa ndondocha. Hii ni nchi ya ajabu mimi leo nipo hapa kuliandaa Taifa.. kule Afrika Kusini juzi, jana aliyekuwa Rais Jacob Zuma amelazimishwa kujiuzulu, Mugabe kang’olewa…. Magufuli ni mwepesi kama karatasi’.

Mbowe pia anadaiwa siku hiyo kwenye viwanja hivyo akiwa amejumuika na wengine ambao hawapo mahakamani aliwashawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali.

Kwa upande wa mchungaji Msigwa anadaiwa siku hiyo kwenye viwanja hivyo aliwashawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa ambao wanatetewa na mawakili Peter Kibatala na Hekima Mwesigwa, walikana kutenda makosa hayo.

Wakili Faraja akiwakilisha Jamhuri  alidai upelelezi umekamilika  kama mahakama itapendezwa kesi hiyo ipangiwe usikilizwaji wa awali leo au kesho kama ratiba ya mahakama itaruhusu.

Nchimbi aliomba kuwasilisha maombi chini ya kifungu cha 392 (A) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Alidai ombi hilo ni la kupinga dhamana ya washtakiwa wote kwa sababu za msingi ambazo aliziwashilisha pamoja na Dk. Zainabu.

Sababu za Jamhuri kupinga dhamana

Wakili Dk. Zainabu alidai wanaomba washtakiwa wasipewe dhamana kwa sababu ya usalama wa jamii  na nchi kwa ujumla wake kwa kuangalia makosa waliyoshtakiwa nayo kama hati ya mashtaka inavyoeleza.

“Upande wa Jamhuri tunatambua dhamana ni haki ya washtakiwa lakini hakuna haki isiyokuwa na wajibu. Moja wapo ya wajibu wa wananchi wa Tanzania kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho, Ibara ya 26 (1) kwamba kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii sheria za nchi.

“Mashitaka yanayowakabili washtakiwa yanaashiria wao kutotii wajibu wao kikatiba, utekelezaji wa haki binafsi unapaswa kuzingatia haki za umma. Kutumia haki ya mtu mmoja kunapaswa kuhakikisha haki za watu wengine haziingiliwi wala kukatizwa,” alidai Dk. Zainabu.

Wakili Dk Zainabu  alidai mipaka hiyo kwa ajili ya haki na uhuru binafsi inapatikana katika Katiba kwenye Ibara ya 30 (1) ambayo inaweka mipaka ya mtu kutumia haki zake zilizoko katika  Katiba.

Alidai makosa wanayoshtakiwa nayo washtakiwa yanahatarisha usalama wa umma wa Watanzania, hivyo wakipewa dhamana watapata nafasi ya kuendelea kufanya makosa hayo,

Dk. Zainabu alidai wanatambua jukumu la kutoa dhamana lipo chini ya mamlaka ya mahakama lakini kabla ya mahakama kutumia mamlaka yake ya kutoa dhamana ama kuzuia inapaswa kuzingatia mazingira ya kosa husika.

Alidai katika kufanya hivyo mahakama inaongozwa na matakwa ya haki, ambapo kwenye hilo wanaiomba mahakama izingatie masilahi ya umma kwa ujumla wake, hatari ya makosa ambayo washitakiwa wanakabiliwanayo na usalama wa taifa kwa ujumla wake.

Katika kuwasilisha sababu hizo, Wakili Dk. Zainabu na Nchimbi, walitumia uamuzi wa kesi za Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kibatala aomba dhamana

Kwa upande wake Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliiomba mahakama kuwapatia washtakiwa dhamana kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yanadhaminika.

Alidai washtakiwa hao hawajashtakiwa kwa sheria ya usalama wa Taifa ambayo haina dhamana, hivyo aliomba wapewe dhamana.

“Hakuna ushahidi wala kiapo wa hayo yote yaliyoelezwa na upande wa Jamhuri  kutaka kupinga dhamana na tukitaka kutenda haki taarifa hizo ziwasilishwe kwa njia ya kiapo.

“Hakuna chochote kilichozungumzwa na upande wa Jamhuri cha kisheria, ila wao wamewasilisha hoja tu na sheria haitoki hewani ina maelekezo yake na msingi wake mkubwa katika kifungu cha 148 cha CPA.

“Kifungu hicho kinazungumzia mamlaka ya mahakama hiyo ya kutoa dhamana na mashtaka yanayostahili kwa mshtakiwa kupewa dhamana. Kitu peke kilichomo ni usalama wa washtakiwa.

“Hoja za upande wa Jamhuri ni kama mahakama itoe adhabu lakini sheria haielekezi hivyo na  hakuna mawakili wa Serikali aliyeeleza tangu Februari 16, mwaka huu mpaka wanafikishwa mahakamani walikuwa wapi,” alidai.

Alidai washtakiwa hao wanaishi maeneo mbalimbali Goba, Sinza na Mikocheni hivyo upande wa Jamhuri hawajaeleza usalama wanaohatarisha ni wa maeneo gani.

POLISI

Awali, kabla ya kupandishwa kizimbani, viongozi hao walifika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam saa 3:00 asubuhi ikiwa ni mwendelezo wa kutakiwa kufika kituoni hapo kwa ajili ya kusubiri kinachoendelea.

Ilipofika saa 5:00 viongozi hao walipelekwa kwenye Ofisi za Naibu Kamishna wa Kanda Maalumu kwa ajili ya kusubiri maelekezo.

Baada ya hapo, waliwekwa mahabusu huku wakitakiwa kuvua viatu, mikanda, saa na vitu vingine ambavyo walikuwa navyo na kuvikabidhi kwa madereva wao pamoja na viongozi wengine wa chama hicho waliokuwepo maeneo hayo.

Kwa upande wake Esther Matiko alivua kitenge alichokuwa amevaa na kukabidhiwa kwa dereva wake ili aweze kuvirudisha nyumbani.

Hata hivyo, Heche na Mdee hawakuwepo kituoni hapo licha ya kutakiwa kuripoti kama viongozi wengine.

Pia katika tuhuma hizo amejumuishwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye awali hakuwamo katika orodha ya viongozi waliotakiwa kuripoti polisi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles