29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mpango wa kuendeleza malisho nchini utainua sekta ya mifugo


Na Ismail Ngayonga-MAELEZO 

SEKTA ya Mifugo imeendelea kutoa mchango muhimu katika uchumi wa wananchi wa vijijini na Tanzania kwa ujumla, ambapo bidhaa zake zikiwemo nyama, maziwa, ngozi na mbolea zikiendelea kuuzwa nje ya nchi na kuchangia katika Pato Ghafi la Taifa.

Mifugo inachangia asilimia 30 ya Pato Ghafi la Kilimo la Taifa, ambapo katika mwaka 2017, sekta ya mifugo ilikua kwa asilimia 2.8 ikilinganishwa na asilimia 2.6 mwaka 2016 na kuchangia asilimia 6.9 katika pato la Taifa.

Eneo la Tanzania Bara lina ukubwa wa hekari milioni 94.5 lenye matumizi mbalimbali ya ardhi ikiwa ni pamoja na makazi ya binadamu, miundombinu, kilimo, ufugaji na eneo la kuchungia, misitu, wanyamapori, uchimbaji wa madini.

Kulingana na takwimu zilizokokotolewa katika Mpango Kabambe wa Mifugo Tanzania, katika mwaka 2017 idadi ya mifugo nchini inakadiriwa kufikia ng’ombe milioni 30.5, mbuzi milioni 18.8 na kondoo milioni 5.3, kuku wa asili milioni 38.2, nguruwe milioni 1.9 na punda wapatao 595,160.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, inahitaji wastani wa hekta 2 za ardhi ya kulishia kila mwaka kwa kila mfugo mmoja na hivyo kuhitajika jumla ya hekta milioni 57.6, ambayo ni wastani wa asilimia 64 ya ardhi yote ya Tanzania Bara, ambapo maeneo mengi ya ardhi ya malisho yameingizwa katika ufugaji na mfumo wa kilimo cha ufugaji kama nyanda za malisho.

Nyanda za malisho ni rasilimali muhimu katika uzalishaji wa mifugo na kuweka mfumo jumuishi wa mifugo katika misimu ya mvua, ukame, maji na uhamaji ili kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi na hivyo kuondoa ugumu wa kuyapata maeneo mapya na taratibu za usimamizi.

Akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa  mwaka 2018/19, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, anasema katika mwaka 2017/18, Serikali Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi imetenga jumla ya hekta 10,378.53 kwa ajili ya maeneo ya ufugaji katika vijiji 13 katika wilaya za Makete, Kilolo, Tanganyika, Mpanda na Kalambo.

Waziri Mpina anasema hadi kufikia mwezi Juni, 2017, jumla ya vijiji 1,695 vilikuwa vimepimwa na kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kati ya vijiji 12,545 vilivyopo nchini, ambapo jumla ya hekta milioni 2.545 zimetengwa kwa ajili ya ufugaji katika vijiji 741 vilivyoko katika mikoa 22.

Anaongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, asasi zisizo za Kiserikali na wadau wengine imeendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa ardhi kuhusu mipango ya matumizi bora ya ardhi kupitia mradi wa usimamizi endelevu wa nyanda za malisho kwa ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).

“Elimu imetolewa kwa wafugaji wa vijiji vya Leluku, Ngapapa na Olkitkit katika Wilaya ya Kiteto. Aidha, mafunzo kuhusu utatuzi wa migogoro kati ya wafugaji na wakulima yalitolewa kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Kilindi, Handeni, Bagamoyo, Chalinze, Chamwino, Chemba, Kiteto, Kondoa na Morogoro,”  anasema Mpina.

Akifafanua zaidi Waziri Mpina anasema katika mwaka 2017/18 Serikali imeongeza uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za malisho katika mashamba ya Serikali na sekta binafsi, ambapo jumla ya tani 10 za mbegu bora za malisho zilizalishwa kutoka mashamba ya Serikali na Sekta Binafsi ikilinganishwa na tani 3.717 zilizozalishwa mwaka 2016/2017.

Kwa mujibu wa Mpina, Serikali imetoa elimu ya uzalishaji na hifadhi ya malisho ikiwa ni pamoja elimu ya unenepeshaji mifugo imetolewa kupitia runinga ilitolewa kwa wananchi katika vijiji vya Wilaya ya Mvomero (Mkindo, Hembeti, Dihombo Kigugu), Kilosa (Rudewa, Gongoni na Pepea) na Wilaya ya Babati (Mawemairo, Matufa, Seloti, Singu na Gichameda.

Akifafanua zaidi, Waziri Mpina anasema Serikali pia ilifanya ukaguzi wa maeneo 72 ya kuzalisha, kuhifadhi na kuuza vyakula vya mifugo, ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilisajili viwanda 26 vya kutengeneza vyakula vya mifugo na maeneo matano (5) ya kuhifadhi na kuuza vyakula hivyo.

“Katika mwaka 2018/2019, Wizara itaendelea kusimamia na kudhibiti ubora katika uzalishaji na usindikaji wa vyakula vya mifugo nchini kwa kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa vyakula vya mifugo 50 na watengenezaji wa vyakula vya mifugo 40 na kuendelea kukagua maeneo na viwanda vya kusindika vyakula vya mifugo,” anasema Waziri Mpina.

Aidha, Waziri Mpina anasema katika mwaka 2018/19, Serikali itaendelea kuhamasisha na kuelimisha wafugaji na wawekezaji kuhusu mfumo wa kuzalisha, kuhifadhi, kusindika malisho na vyakula vya mifugo kwa kuanzisha mashamba darasa katika wilaya 10 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Tabora, Simiyu, Mara, Geita, Mbeya na Kagera.

Uchoraji wa ramani ya rasilimali za nyanda za malisho ni nyenzo muhimu kutumika katika mchakato wa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima wafugaji, kwa kuwa unatoa taarifa za kutosha na hivyo kupunguza uwezekano wa migogoro ya matumizi ya ardhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles