25 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Tunawapongeza askari hawa kwa kazi nzuri

ASKARI polisi sita mkoani Mwanza juzi wameuaga mwaka 2018 kwa furaha baada ya Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Simon Sirro kuwapandisha vyeo kutokana na kazi nzuri waliyofanya.

Tunasema wamefunga vizuri kwa sababu inawezekana hawakutegemea kupata vyeo hivyo mwishoni mwa mwaka, lakini utendaji kazi wao mzuri na kutimiza majukumu yao kwa wakati ndiyo sababu ya kufunga mwaka kwa furaha.

Tunasema ni jambo jema ambalo limefanywa na IGP Sirro kuwapandisha vyeo wapiganaji hawa ambao walijitoa kwa kila namna kukabiliana na majambazi ambao walikuwa na silaha kali zikiwamo za kivita.

Tukio la askari hawa kuvishwa vyeo vipya lilifanywa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Jonathan Shana kwa niaba ya IGP.

Tunarudia kusema ushujaa wa wapiganaji hawa ni kielelezo tosha kuwa wako tayari kulitumikia taifa

Tunatambua askari hawa wamepata ofa hiyo baada ya utendaji kazi mzuri, huku mmoja akipatiwa cheti cha heshimna na utendaji bora kutokana na kufaulu vizuri katika mafunzo ya taaluma mbalimbali ndani ya jeshi hilo.

Askari waliotunukiwa vyeo ni WP. 12415 Dominika Nnko, G.4745 Rodrick Ndyamukama, G.7087 na Thomas Masingija ambao walikuwa konstebo na sasa wanakuwa koplo.

Wengine ni F5820 Amon Rubanzibwa na F.8361 Belson Sanga ambao wamepandishwa kutoka koplo kuwa sajenti na kukabidhiwa Sh 40,000 kila mmoja.

Lakini pia Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, ASP Levina Jeremia aliyepandishwa cheo na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni Dar es Salaam alikabidhiwa cheti cha shukrani na fedha Sh 800,000 kama sehemu ya kutambua mchango wake katika mafunzo aliyoshiriki ndani na nje ya nchi na kufaulu vizuri.

Tunakubaliana na Kamanda  Shanna kuwa askari hao wamekuwa mstari wa mbele katika kutimiza wajibu wao kitendo ambacho kinapaswa kuigwa na askari wengine ambao wamekula kiapo cha kulitumikia taifa usiku na mchana.

Tunasema hivyo kwa sababu ushujaa uliooneshwa na askari hawa ambao waliamua kuweka kando uhai wao, unapaswa kuwa kielelezo tosha kwa wapiganaji wetu wengine ambao kwa namna moja au nyingine ni wavivu.

Uadilifu huu ni kielelezo tosha cha wapiganaji ambao wamelijengea heshima kubwa Jeshi la Polisi ambao kwa nyakati tofauti limekuwa likikumbwa na tuhuma za rushwa na utovu wa nidhamu.

Tunasema uadilifu huu unapaswa kuwa endelevu na silaha ya kila mpiganaji kwa maana tunatambua askari siku zote wamejitolea maisha kwa ajili ya Watanzania, hivyo tunasema kupandishwa vyeo huku kuwape morali zaidi.

Tunasisitiza hili kwa sababu kupata cheo cha ukoplo au usajenti kusiwafanye wakabweteka na kushindwa kuendeleza uadilifu walioonesha kwa taifa lao. Lakini wakati tunawapongeza wapiganaji hawa, tunamshauri IGP Sirro mbali ya kuwapatia vyeo, tunasikitishwa na kiasi kidogo cha fedha walichopewa wapiganaji hawa ambacho hakiendani na ukubwa wa matukio waliyoshiriki.

Sh 40,000 ni kiasi kidogo kulingana na uzito wa tukio lenyewe. Kwa vile Kamanda Shana ni mwelewa, tunategemea anaweza kuwapa hata motisha nyingine.

Tunamalizia kwa kusema polisi Mwanza mmeonesha mnaweza, endeleeni kuchapa kazi, mnatimiza wajibu wenu vizuri kwa kuzingatia uadilifu na utawala bora. Tunawapongeza wapiganaji kwa kazi nzuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles