JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA UTAFITI
BARA la Afrika ndilo linalosifisika kuwa na wanyama wengi wakubwa kwa wadogo kuliko lingine lolote lile duniani kwa sasa.
Lakini miaka 13,000 iliyopita Bara la Amerika ya Kaskazini lilikuwa na mamalia wengi zaidi kuliko waliopo katika Afrika hii ya sasa.
Naam tumelinganisha Amerika Kaskazini ile ya kale dhidi ya Afrika hii ya sasa, kwa vile Afrika ya zama hizo haifanani na hii, ambayo wanyama wanazidi kutoweka kutokana na sababu mbalimbali kama tutakavyoona baadaye.
Katika Amerika ya Kaskazini ya zama zile kulikuwa na kila aina ya mamalia kama vile punda, farasi, ngamia na mnyama aliyetoweka aitwaye Glyptodon, ambaye alifanana na kuwa na ukubwa sawa na gari aina ya Volkswagen Comb.
Smilodon, aina ya jamii ya paka mwenye ukubwa kama simba wa sasa wa Afrika alitawala nyasi za bara hilo.
Pia kulikuwa na mnyama wa urefu wa futi saba kwenda juu ambaye aliweza kukata matawi makubwa ya miti.
Na aina hiyo ya viumbe hawa wakubwa si tu walipatikana Amerika ya Kaskazini, bali katika kila bara na mamalia hawa kwa wastani walikuwa wakubwa mno wakati wakiishi miaka kuanzia milioni 2.5 hadi 11,700 iliyopita.
Wanasayansi kwa muda mrefu wamekuwa katika mjadala juu ya sababu ya kutoweka kwa viumbe hawa huku wale wenye maumbo madogo wakinusurika.
Timu ya watafiti walioongozwa na mwanabiolojia wa Chuo Kikuu cha New Mexico nchini Marekani, Felisa Smith walichambua ushahidi kutoka mamilioni ya miaka ya mamalia waliotoweka.
Walibaini kuwa kwa kila bara mamalia wakubwa walianza kufa kipindi kile kile wanadamu wa kwanza alipoanza kujitokeza.
Walitangaza matokeo yao katika Jarida la Sayansi Alhamisi ya wiki iliyopita.
Iwapo mwelekeo wa mtokomeo huo utaendelea kwa kasi hii wanyama wa kizazi cha sasa kama vile tembo, faru, twiga, kiboko, tiger, nyati na mamalia wengine wakubwa kama hao watatoweka, kwa kadiri tishio kutoka kwa wanadamu linavyoongezeka.
Tishio hilo linatokana na uwindaji wa kupitiliza, ujangili au aina nyingine za mauaji yasiyo ya moja kwa moja yanayotokana na shughuli za binadamu katika misitu.
Kwa kitisho hicho dhidi ya mamalia wakubwa kipindi cha miaka 200 ijayo itamuacha ngombe, mamalia afugwaye na binadamu kama mnyama pekee mwenye mwili mkubwa atakayesalia duniani, watafiti wanaonya.
Utafiti huo unabainisha kuwa ongezeko la watu katika maeneo mbalimbali duniani linachangia kitisho hicho kutokana na shughuli za kibinadamu.
Utafiti huo wa kisayansi umebainisha kuwa kwa sasa Afrika likiwa eneo lenye unafuu duniani linapokuja uwingi wa wanyama kulinganisha na mabara mengine, kuenea kwa binadamu duniani miaka zaidi ya 1,000 iliyopita kunatishia uwepo wa wanyama wakubwa.
Tisho hilo linamfanya ng’ombe kuwa mnyama mkubwa pekee atakayebakia duniani katika muda wa karne chache zijazo.
Kuenea na homoni za binadamu wa kale wenye spishi kama za Neanderthals kutoka Afrika kunasababisha kupotea kwa wanyama hao wakubwa, watafiti wanasema.
Smith aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna mfano wa wazi sana wa ukubwa wa uharibifu unaofuatia uwepo wa homoni kutoka nje ya Bara la Afrika.
Wanadamu waliwawinda wanyama wakubwa kwa ajili ya kupata kitoweo cha nyama na wakati viumbe vidogo kama vile panya vilitoroka na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya kuchunguza mwenendo wa wanyama zaidi ya miaka 12,500.
Lakini ujio wa wanadamu duniani unaweza kuwa sababu ya mtoweko huo? Wengine wanadai kwamba mchawi mkubwa wa mtoweko huo wa wanyama ni mabadiliko ya tabianchi.
Lakini katika utafiti wao mpya Smith na timu yake walikusanya data za wanyama wote wakubwa walioishi kuanzia miaka 65 iliyopita hadi leo hii.
Waligawanya katika kalenda ya matukio ya miaka milioni moja moja na kuchambua mwelekeo wa mtoweko wa kila mmoja wa wanyama hao.
“Tulibaini kwamba mabadiliko ya tabia nchi hayakuhusika na mtoweko wa mamalia kipindi cha miaka zaidi ya milioni 65 iliyopita,” anasema.
Lakini kuanzia miaka 125,000 iliyopita hadi leo hii, mamalia wenye miili mikubwa wanaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kutoweka kuliko wale wenye miili midogo, utafiti umebainisha.
Wastani wa ukubwa wa mamalia wanaonusurika umepungua kutokana na matokeo hayo, na mamalia wenye miili mikubwa wanaonekana wametoweka zaidi wakati wa ujio wa wanadamu.
Katika Bara la Amerika ya Kaskazini kwa mfano, sehemu kuu ya ardhi, wanyama kwa ajili ya nyama wamepungua uzito hadi kufikia kilogramu 7.6 kutoka uzito wa kilogramu 98 baada ya binadamu kuwasili.
Timu ya utafiti kutoka Marekani iliandika kwamba kama hali hii ikiendelea mnyama mkubwa pekee atakayebaki katika miaka 100 ijayo ni ng’ombe wa kufugwa mwenye uzito wa kilogram 900, na hiyo inamaanisha viumbe vingine ambavyo ni wanyama wakubwa kama vile twiga, tembo na viboko watapotea.
Machi mwaka huu, faru mweupe wa mwisho kabisa duniani alifariki dunia nchini Kenya na kuongeza wasiwasi wa mtoweko wa viumbe adimu wanaolindwa sana kwa sasa.
Lakini tafiti zingine zinaonesha shaka juu ya kuendelea kufa kwa wanyama wengine licha ya kuwepo juhudi za hifadhi ya kuzuia vitisho kwa wanyamapori kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, kupotea kwa misitu, uchafuzi wa mazingira na ukuaji wa miji.
Thomas Brooks, mwanasayansi mkuu kutoka Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Viumbe Asilia (IUCN), ambaye hakuhusika katika utafiti huo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa utafiti mwingine unaonesha wanyama wakubwa kama tembo wanaweza kufaidika katika maeneo yaliyohifadhiwa kuliko wanyama wadogo.
Orodha ya aina za wanyama zilizohifadhiwa na ICUN inawataja wanyama hao wa porini wenye ukubwa unaolingana na ng’ombe kama vile nyati wa Afrika, kuwa sasa wapo hatarini kupotea.
Utafiti wa kisayansi pia huhusisha wanyama wa baharini kama vile nyangumi wa bluu kiumbe kikubwa zaidi cha baharini kilichobakia kwa sasa.
“Mimi ningependa kusema kwamba matumaini yangu hayawezi kupotea kwa sababu ninawapenda tembo, lakini idadi ya wanyama wengi wa ardhi ilishuka,” anasema Thomas Brooks.